Kolombia: Wanawake wamejiingiza katika biashara ya kukodisha tumbo kwa ujauzito

Mwanamke anakubali kukodisha tumbo lake ili kubeba mimba isiyo yake kwa shilingi laki 5 tu pesa za Kenya.

Muhtasari

• Nchini Kolombia, wanawake wengi wanaweka mabango wakitangaza biashara zao za kukodisha tumbo kwa ajili ya kuwabebea watu ujauzito.

• Hakuna sheria inayozuia biashara ya uuzaji na ununuzi wa watoto katika taifa hilo la Amerika ya Kusini.

Image: Maktaba

Wakati biashara ya kuuza na kununua watoto ni marufuku katika mataifa mengi nchini, suala hilo ni biashara ya kawaida tu katika taifa la Kolombia, Amerika Kusini.

Kulingana na jarida moja la kitaifa, Kupata mwanamke wa kukukodishia tumbo lake kwa ajili ya mtoto (surrogacy) nchini Kolombia ni rahisi kama kununua au kuuza gari la mitumba katika matangazo yaliyoainishwa.

Vigezo vya kupata mtu huyo wa kukukodisha tumbo kwa ajili ya kukuzalia ni vipi?

Kulingana na jarida hilo, unachohitaji ni kuwa tu na simu yenye uwezo wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii, na haswaa mtandao wa Facebook.

Kule utaona matangazo ya kila aina ambayo yamewekwa tena kwa wino uliokolewa, “Surrogate kwa ajili ya kukodisha, mimi ni mama kutoka Kolombia. Nina nia ya kukodisha tumbo langu kwa ajili ya kukubebea mimba yenye nguvu na afya nzuri, mimba isiyoweza kuwa na matatizo.”

Kulingana na jarida hilo meseji kwenye matangazo ya kukodisha tumbo kwa ajili ya mimba nchini humo yanapishana na kubishana utadhani ni wafanyibiashara wa nguo za Mitumbo katika soko la Gikomba jijini Nairobi kila mmoja akitangaza bei na ofa za nguo zake kwa wateja wanaofurika na kusukumana kwenye vijia vyembemba sokoni humo.

“Kwenye tovuti hizo hizo za matangazo ya wauza tumbo kwa mimba, wanunuzi huweka wazi matakwa yao. Kwa ujumla, wahusika wanatafuta kile ambacho mteja yeyote angetafuta katika tangazo lililoainishwa: ubora mzuri kwa bei nzuri,” jarida hilo linaripoti.

Nchini Kolombia, kununua watoto kwa njia ya kukodisha tumbo kunazidi kuwa jambo la kawaida. Zoezi hili - ambalo limepigwa marufuku katika mataifa mengi ya Ulaya kama vile Uhispania, Ufaransa, Ujerumani na kwingineko - halidhibitiwi nchini Kolombia. Mashirika na kliniki nyingi huchukua fursa ya ombwe hilo la kisheria kufanya biashara.

Wanawake nchini humo ambao sasa wamechukua fursa hiyo kama nafasi ya kupata utajiri kwa haraka, walisema huwa wanakubali kubebea mtu ujauzito kwa malipo ya dola elfu 4 tu ambazo ni sawa na shilingi laki tano ama ukipenda nusu milioni tu pesa za Kenya.

Kolombia ina aina mbili za uzazi wa aina hiyo (surrogacy): katika moja, mwanamke mjamzito hana uhusiano wa maumbile na kiinitete, ambayo ni, yai lililorutubishwa ni la mwanamke mwingine na mjamzito kazi yake ni kubeba na mpaka pale mtoto atakapozaliwa baada ya miezi 9.

Aina nyingine ya surrogacy ni ngumu zaidi: surrogate hutoa yai lake mwenyewe na linarutubishwa. Zoezi hili la mwisho linahusisha matatizo mengi ya kisheria kwamba, licha ya ukweli kwamba ni fursa ya ziada ya biashara, mashirika mengine yanaipiga marufuku.