Kenya kuchunguza madai ya unyanyasaji wa kingono katika mashamba ya chai

Kampuni hizo zinasema kuwa zimewasimamisha kazi wasimamizi watatu wanaohusika.

Muhtasari

•Bunge limetaka uchunguzi ufanyike kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono kwenye mashamba ya chai taarifa iliyoripotiwa na BBC.

•Mbunge Beatrice Elachi alisema ni bahati mbaya kwamba visa kama hivyo bado vinaendelea.

Image: BBC

Bunge la Kenya limetaka uchunguzi ufanyike kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono kwenye mashamba ya chai taarifa iliyoripotiwa na BBC.

Mbunge Beatrice Kemei alisema aliitazama ripoti hiyo kwa "mshtuko mkubwa".

BBC ilibaini kuwa zaidi ya wanawake 70 walikuwa wamenyanyaswa na wasimamizi wao kwenye mashamba yanayoendeshwa na makampuni mawili ya Uingereza - Unilever na James Finlay.

Kampuni hizo zinasema kuwa zimewasimamisha kazi wasimamizi watatu wanaohusika na wao pia wanashangazwa na madai hayo.

Wakfu wa Fairtrade ulieleza madai hayo kuwa "ya kuchukiza", na kusema uchunguzi wa BBC Africa Eye na BBC Panaroma - "haikuwa zaidi ya kampeni mtandaoni inayoitwa #MeToo moment for tea".

Bi Kemei, ambaye ni mwakilishi wa wanawake katika eneo linalolima chai katika kaunti ya Kericho, alisema ripoti hiyo iliangazia unyanyasaji wa kijinsia "uliokithiri" kwa "mashirika mengi ya kimataifa ya chai yanayofanya kazi nchini mwetu".

Mbunge Beatrice Elachi alisema ni bahati mbaya kwamba visa kama hivyo bado vinaendelea.

"Leo ni siku ngumu sana kwangu kama mwanamke, kiongozi na raia wa Kenya.

Leo nimekumbushwa kuwa utumwa bado upo katika taifa hili; siwezi kueleza jinsi mwanaume amewadhulumu wanawake kwenye mashamba ya chai kwa miaka 30 na hakuna chochote, kimefanywa," alinukuliwa na vyombo vya habari vya ndani akisema.

Naibu Spika Gladys Shollei aliagiza kamati ya wabunge kukamilisha uchunguzi kuhusu madai hayo ndani ya wiki mbili.

Katika uchunguzi wa BBC, mwanamke mmoja alisema alikuwa ameambukizwa VVU na msimamizi wake, baada ya kushinikizwa kufanya naye mapenzi.

Mwanamke mwingine alisema meneja wa kitengo alimsimamisha kazi hadi akakubali kufanya mapenzi naye.