Mwanamume aishi kwa siku 31 kwa kula wadudu

Jhonattan Acosta, 30, alitengana na marafiki zake wanne walipokuwa wakiwinda kaskazini mwa Bolivia.

Muhtasari
  • Hatimaye Bw Acosta alipatikana na kikundi cha watafutaji kilichoundwa na wenyeji na marafiki mwezi mmoja baada ya kutoweka

Mwanamume mmoja wa Bolivia ameeleza jinsi alivyoweza kuishi kwa siku 31 katika msitu wa Amazon baada ya kupotea.

Jhonattan Acosta, 30, alitengana na marafiki zake wanne walipokuwa wakiwinda kaskazini mwa Bolivia.

Anasema alikunywa maji ya mvua yaliyokusanywa kwenye viatu vyake na kula minyoo na wadudu huku akijificha dhidi ya chui wakali na peccaries, aina ya mamalia wanaofanana na nguruwe.

Hatimaye Bw Acosta alipatikana na kikundi cha watafutaji kilichoundwa na wenyeji na marafiki mwezi mmoja baada ya kutoweka.

"Inashangaza, siwezi kuamini kuwa watu waliendelea na utafutaji huo kwa muda mrefu," alisema huku akitokwa na machozi.

"Nilikula minyoo, nilikula wadudu, huwezi kuamini yote niliyopaswa kufanya ili kuishi wakati huu wote," aliiambia Unitel TV. Pia alikula matunda ya mwituni sawa na mapapai, yanayojulikana kienyeji kama gargateas.

"Namshukuru Mungu sana, kwa sababu amenipa maisha mapya."

Familia yake ilisema kuwa bado italazimika kuunganisha maelezo yote ya jinsi Bw Acosta alivyopotea na jinsi alivyoweza kusalia hai lakini wangemuuliza taratibu kwani bado alikuwa ameumia kisaikolojia baada ya tukio hilo.

Bw Acosta alipungua uzito wa kilo 17 (lb 37), kifundo cha mguu kiliteguka na kukosa maji mwilini alipopatikana lakini kulingana na waliompata, bado aliweza kutembea huku akichechemea.

"Ndugu yangu alituambia kwamba alipoteguka kifundo cha mguu siku ya nne, alianza kuhofia maisha yake," Horacio Acosta aliambia gazeti la Página Siete la Bolivia.

"Alikuwa na cartridge moja tu kwenye bunduki yake na hakuweza kutembea, na alifikiri hakuna mtu ambaye angemtafuta tena," Horacio Acosta, mdogo wa manusura, aliongeza.

Jhonattan Acosta hakuwa na panga wala tochi alipopotea na ikabidi atumie buti zake kukusanya maji ya mvua ili kunywa.

Pia aliwaambia jamaa zake kwamba alikutana na wanyama pori akiwemo jaguar.

Ndugu yake mdogo anasema kwamba Jhonattan alitumia cartridge yake ya mwisho kuwatisha kundi la wanyama wa porini, wanyama wanaofanana na nguruwe wanaopatikana katika misitu ya mvua ya Amerika Kusini.

Baada ya siku 31, aliona kundi la watafutaji umbali wa mita 300 (futi 980) na kuchechemea kuelekea kwao kupitia vichaka vyenye miiba, huku akipiga kelele ili kumvutia.

Horacio Acosta anasema kwamba kaka yake alipatikana na watu wanne wa eneo hilo. "Mwanaume mmoja alikuja mbio kutuambia wamempata kaka yangu. Ni muujiza."

Kulingana na Acosta mdogo, Jhonattan ameamua kuacha kuwinda kwa manufaa baada ya mateso yake.

"Atacheza muziki wa kumsifu Mungu. Alimuahidi Mungu hivyo, na nadhani atatimiza ahadi yake," alisema kuhusu kaka yake anayepiga gitaa.

Wakati huo huo polisi walisema watawahoji marafiki wanne wa manusura ili kuelewa jinsi alivyotengana nao.