Mombasa: Mtoto wa miaka 14 atekwa nyara na kuuawa kwa kucharangwa mapanga

Mvulana huyo ambaye alikuwa mtahiniwa wa KCPE mwaka huu alitumwa dukani na mamake majira ya saa mbili usiku lakini hakuwahi rudi hadi pale mwili wake ulipopatikana umekatwa kwa panga.

Muhtasari

• Siku ya Alhamisi mwili wake ulisafirishwa hadi nyumbani kwa  babu yake Masogalini kata ndogo ya Kibwezi mashariki kwa mazishi

Kisu cha mauaji
Kisu cha mauaji
Image: Maktaba//The Star

Familia moja katika kaunti ya Mombasa inalilia haki kutendeka baada ya mtoto wao wa miaka 14 kutekwa nyara na watu wasiojulikana kisha baadae mwili wake kupatikana ukiwa umecharangwa mapanga.

Kennedy Maluni, kijana mwenye umri wa miaka 14 ambaye alikuwa mtahiniwa wa mwaka huu katika mtihani wa KCPE alikuwa ametumwa na mamake dukani majira ya saa mbili usiku lakini hakuwahi rejea nyumbani hadi pale mwili wake ulipopatikana umekatwa katwa kwa panga siku chache baadae.

 

Siku ya Alhamisi mwili wake ulisafirishwa hadi nyumbani kwa  babu yake Masogalini kata ndogo ya Kibwezi mashariki kwa mazishi

Kennedy alikatwakatwa na panga na majambazi Mwamlai,kaunti ndogo ya jomvu Mombasa tarehe 23 Agosti

Mamake mzazi Margret Mbithe alisema kuwa alitarajia kuwa katika umri wake wake wa uzee mtoto wake Kennedy angemusaidia ila imebaki kuwa kilio kwake kwa kuwa watu ndio wanamusaidia ikiwemo kampuni ya usambazaji saruji ya Mombasa ndio inamusaidia kurudisha mwili wa mtoto wake nyumbani.

Mbithe anasema kuwa hatapumuzika mpaka pale waliotekeleza kitendo hicho cha unyama kwa mwanawe watakapotiwa hatiani na kuhukumiwa.

Walimu katika shule ya Vision of Hope Educational Center walimtaja Kennedy kama mwanafunzi aliyetia bidii kwa masomo yake.

Alhamisi wanaharakati wa haki za binadamu ,makasisi,na mabalozi wa haki za watoto walisema kuwa Kennedy anafaa kupata haki huku wakiomba  polisi kuchunguza kisa hicho na kuwatia mbaroni wote na ambao waliusika na kifo cha mtoto mdogo wa shule kwa kukatisha uhai wake .

Mkuu wa polisi wa jomvu Lydia Wanjiru amesema kuwa maafisa wa upelelezi wamewakamata watu watatu wanaosaidia upelelezi.