Linapokuja suala la kutambua ugonjwa kwa usahihi, unaweza kufikiri mara zote unahitaji mashine za gharama kubwa na vifaa vinavyoweza kuangalia kwa undani kile kinachotokea katika mwili.
Ingawa vyombo hivi vinafanya kazi ya kushangaza, lakini sio pekee vinavyoweza kugundua magonjwa. Kuna matukio mengi ambapo wamiliki wa wanyama hugundua kwamba walikuwa na tatizo la kiafya kwa sababu ya wanyama wao.
Mifano hii, ni pamoja na mbwa kulamba, kunusa, na hata kujaribu kutafuna madoa kwenye ngozi ya wamiliki wao, ambayo baadaye hugunduliwa kuwa ni saratani ya ngozi.
Hawa ni baadhi ya wanyama ambao wanaweza kugundua maradhi kwa wanadamu.
Mbwa
Huenda ni mfano unaojulikana zaidi wa mnyama anayeweza kutambua magonjwa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kutetemeka kutokana na shida ya ubongo, saratani ya kibofu cha mkojo na malaria.
Kifafa na kiwango cha chini cha sukari katika damu kwa wagonjwa wa kisukari vinaweza pia kufichuliwa na mbwa maalumu waliofunzwa.
Uwezo wa mbwa wa kutambua harufu ni muhimu katika kutambua harufu fulani, hata ile ya kiwango kidogo. Inaaminika uwezo wa mbwa wa kunusa harufu, ni mara 10,000 zaidi ya uwezo wa binaadamu. Wanaweza hata kutumia pua zao kuchunguza harufu mpya.
Mbwa wa tahadhari hufunzwa kutambua mabadiliko ya harufu au mabadiliko ya kimwili na kitabia kwa mlezi wao, ambayo yanatabiri kifafa (au tukio jingine la kiafya).
Mbwa wa utambuzi kwa kawaida husangaa wanapotambua kisha hutangamana na mhudumu wao, wakati mwingine huwapapasa au kuwagusa ili kuashiria wanahitaji kuchukua hatua kwa ajili ya usalama wao.
Panya
Panya wana uwezo mzuri katika kugundua harufu fulani. Wapo panya wamepewa mafunzo ya kutambua harufu ya vilipuzi vya ardhini nchini Msumbiji.
Pia wamethibitika kuwa na uwezo mzuri katika uchunguzi wa kimatibabu, hugundua kifua kikuu katika sampuli za makohozi ya watu wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo.
Panya ni wepesi na huchukua dakika 20 tu kukagua sampuli 100 za wagonjwa. Wanatumia hisia zao za kunusa kugundua dalili za kemikali ya kifua kikuu katika sampuli.
Hilo huwafanya panya hao waliofunzwa kuwa chaguo muhimu pale muda, vifaa na pesa vinapokuwa haba katika hospitali au maabara. Wanatambua kwa usahihi visa vya TB kwa 81%.
Nyuki
Wadudu hawa wanaweza kugundua dalili za magonjwa fulani kupitia sampuli, ikiwa ni pamoja na saratani ya mapafu, kifua kikuu na uviko-19.
Wana uwezo mkubwa wa kunusa harufu ndogo sana, na hilo huwafanya kuwa na uwezo wa kugundua mabadiliko ya kemikali kama vile mbwa na panya.
Uwezo huu huwafanya nyuki kuwa muhimu kugundua magonjwa kwa njia sawa na wanyama wengine. Ukubwa wao unaweza kuwafanya kuwa chaguo bora na la gharama nafuu kwa "uchambuzi" wa haraka wa sampuli.
Wanawezaje kutambua magonjwa?
Wana uwezo wa kugundua mabadiliko madogo katika mfumo wa harufu kupitia kemikali za mtu. Wanaweza kutambua mabadiliko madogo katika kemikali ambayo mwili hutoa kwa viwango vya chini sana, hata wakati mtu akiwa na afya.
Pumzi ya mwanadamu inatoka takribani kemikali za gesi 3,500. Muundo na mkusanyiko wa kemikali ambazo mwili hutoa hubadilika kulingana na afya ya mtu na kemikali hizo hubadilika ikiwa mwili unapigana na maambukizi au kukabiliana na tatizo la kiafya.
Uwezo wao wa kufichua magonjwa kwa usahihi unaweza kuwa njia bora, isiyovamizi, ya haraka na ya gharama nafuu ya kutambua hali fulani. Inaweza hata kuongeza zaidi mwingiliano mzuri kati ya watu na wanyama.
Wanyama wanaotumiwa kutambua magonjwa hutumiwa na vifaa vingine vya matibabu. Lakini ikiwa mifumo ya udhibiti itaruhusu, wanyama hawa siku moja wanaweza kuwa sehemu muhimu ya utambuzi wa magonjwa.
Mfano, mbwa wa kugundua uviko 19, walikuwa wepesi na bei nafuu kuliko vipimo vya kawaida vya PCR. Kwa kuelewa uwezo wa wanyama, tunaweza kuboresha uchunguzi wa maabara.
Ingawa kutumia ujuzi wa kunusa wa wanyama kunaweza kuwa na manufaa kwetu, ni muhimu kukumbuka kwamba afya na ustawi wa viumbe hawa lazima pia vipewe kipaumbele.