• Visa hivi vimezipata idara za dola tope katika jamii ya kimataifa kutokana na jinsi washukiwa sugu wa mauaji wanavyotoweka katika vituo vya polisi vyenye usalama mkali saa 24 kila siku
Kenya imejulikana kama nchi yenye idara nzuri ya ujasuri, ndani ya nje ya Afrika.
Lakini licha ya sifa hii, taifa hili si mara moja limejipata katika mwanga hasi kimataifa kuhusu kutoweka kwa njia tatanishi kwa baadhi ya washukiwa sugu kutoka kwenye seli za polisi.
Katika Makala hii, tunaangazia baadi ya visa vya washukiwa sugu wa mauaji ambao walitoroka seli na kuzipaka tope idara za polisi na ujasusi kimataifa.
Masten Wanjala
Oktoba mwaka 2021, idara ya ujasusi ilisifiwa kwa kufichua moja ya kisa cha kuogofya nchini baada ya kumtia mbaroni kijana Masten Wanjala ambaye baadae alikiri kuhusika katika msururu wa visa vya mauaji ya makumi ya watoto.
Wanjala aliwaambia makachero wa upelelezi kwamba alitekeleza msururu wa mauaji ya watoto na kuzika miili yao katika makaburi yasiyo na vina virefu katika eneo la Kabete.
Ripoti za vyombo vya habari zilionyesha kuwa Wanjala alinakili mauaji yote ya kutisha ambayo anadaiwa kutekeleza, na kuongeza kuwa katika visa vingine, aliripotiwa kunyonya damu kutoka kwa wahasiriwa wake.
Alihusishwa na kifo cha angalau watoto 12.
Kufuatia ungamo lake, Masten Wanjala alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Jogoo Road akisubiri kufikishwa mahakamani lakini siku chache baadae, taifa lilipigwa na butwaa kwa taarifa kwamba ametoroka seli.
Msako mkali dhidi yake ulianzishwa bila kufaulu ambapo baadae alivamiwa na wanakijiji wenye ghadhabu kijijini kwa kaunti ya Bungoma na kuripotiwa kuteketeza mwili wake.
Kutoweka kwake kuliibua maswali mengi si tu nchini bali pia kimataifa ambapo vyombo vya habari vilihoji mazingira ya kutoroka kwake.
Kevin Kang’ethe Kinyanjui
Mwezi Februari mwaka huu, mshukiwa mwingine wa mauaji ya mwanamke nchini Marekani, Mkenya Kevin Kang’ethe alikamatwa nchini baada ya kutoroka Marekani.
Mkenya huyo alikuwa ametangaziwa kutafutwa kwa juhudi zote na polisi baada ya ombi kutoka serikali ya Marekani.
Kang’ethe alikuwa ameshukiwa kutekeleza mauaji ya mwanamke katika uwanja mmoja wa ndege Marekani kabla ya kuabiri ndege na kutorokea mafichoni Kenya.
Baada ya kukamatwa, Kang’ethe alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga akisubiri kusafirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka ya mauaji.
Polisi walisema kuwa mshukiwa ambaye alikuwa amezuiliwa alitoroka na kurukia ndani ya Gari la usafiri wa Umma kabla ya kukimbilia kusikojulikana.
Kutoroka kwake pia kulizua maswali mengi kwa jinsi ambavyo ilielezewa mazingira ya kutoroka kwake na kwa mara nyingine, uzembe uligubika idara ya polisi katika macho ya jamii ya kimataifa.
Msako ulianzishwa na kufaulu baada ya siku kadhaa, ambapo alitiwa mbaroni eneo la Ng’ong.
Collins Jumaisi Khalusha
Mwezi Julai mwaka huu, Kenya iligubikwa na kiza kinene kufuatia vipande kadhaa vya miili ya binadamu kupatikana imetupwa katika timbo la taka chafu la Kware, mtaani Embakasi.
Mnamo Julai 15 2024, maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walimkamata Collins Jomaisi, mshukiwa mkuu wa mauaji hayo.
Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari, mkuu wa DCI Mohamed Amin alidai kuwa Collins, mwenye umri wa miaka 33, alikamatwa katika eneo la Soweto katika kaunti ndogo ya Kayole na anadaiwa kukiri kuwaua wanawake 42, akiwemo mkewe, kati ya 2022 na Julai 11, 2024.
Kulingana na DCI, mshukiwa huyo alidaiwa kufichua kuwa alianza kuua kwa hasira baada ya kumwanzishia mke wake biashara ambapo alikula mtaji.
Mshukiwa huyo alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Gigiri akisubiri kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Hata hivyo, Jumanne ya Agosti 20, taarifa za kutoweka kwake seli ziligonga vichwa vya habari, kuibua swali lile lile la utepetevu kazini kwa maafisa wa polisi.
Kaimu IG wa polisi, Gilbert Masengeli aliwasili katika kituo hicho na kutangaza kusimamishwa kazi kwa muda kwa maafisa 8 wa polisi wakiwemo maafisa wakuu kwa kile alichokitaja kuwa ni kuzembea katika majukumu yao.
Masengeli pia alitangaza kituo cha polisi cha Gigiri kama eneo la uhalifu.
Visa hivi vimezipata idara za dola tope katika jamii ya kimataifa kutokana na jinsi washukiwa sugu wa mauaji wanavyotoweka katika vituo vya polisi vyenye usalama mkali saa 24 kila siku.