Nilifahamu kifo cha binti yangu kupitia mitandao ya kijamii- Mama ya mwanafunzi aliyeuawa Kiambu afunguka

Muhtasari

•Rose Nduta ameeleza kuwa hakuwa amearifiwa kuhusu mauaji ya bintiye kabla ya  habari hizo kuanza kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

•Alifichua kuwa binti yake hakuwahi kumwambia kuhusu mahusiano yake na jamaa anayedaiwa kutekeleza mauaji hayo.

Rose Nduta na bintiye Purity Wangeci aliyeuawa Kiambu
Rose Nduta na bintiye Purity Wangeci aliyeuawa Kiambu
Image: HISANI

Mama ya mwanafunzi wa Kenya Institute of Mass Communication (KIMC) ambaye aliuawa mwezi jana  amefichua kuwa habari za kifo cha bintiye zilimfikia kupitia mitandao ya kijamii.

Purity Wangeci, 19, aliuawa mwezi Mei na mwili wake ambao ulikuwa na majeraha ya kisu na alama za kunyongwa  ukatupwa kando ya barabara iliyo katika eneo la Mburiria, Kiambu.

Mama yake , Rose Nduta ameeleza kuwa hakuwa amearifiwa kuhusu mauaji ya bintiye kabla ya  habari hizo kuanza kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

"Hakukuwa na dalili za kuashiria kuwa kuna jambo linamsumbua. Habari zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii  hata kabla ya habari hizo kufichuliwa kwangu rasmi na polisi. Zilisambaa kote na nikawa mmoja wa waathiriwa wa mitandao ya kijamii," Nduta alisema katika mahojiano na Citizen Digital.

Mama Wangeci alisema alipoona habari za kifo cha bintiye, mwanzoni alitilia shaka kwa kuwa bintiye hakuwa mgonjwa na hakuwa na shida yoyote aliyofahamu kuhusu.

Alisema alikuwa na uhusiano wa karibu mno na binti huyo wake na wangewasiliana mara kwa mara.

"Asubuhi hiyo tulizungumza naye sana. Hata alinitumia video akiwa darasani. Alinionyesha kuwa ametengeza nywele. Tulishiriki mazungumzo rahisi hungedhani ni mama na binti yake," Nduta alisema.

Alifichua kuwa binti yake hakuwahi kumwambia kuhusu mahusiano yake na jamaa anayedaiwa kutekeleza mauaji hayo.

Uchunguzi wa polisi ulibaini kuwa Wangeci aliuawa alipomkabili  mpenzi wake John Wanyoike Kibungi almaarufu VDJ Flexx, baada ya kugundua kuwa yeye ni jamaa hatari.

"Sijui sababu zake kutoniambia. Alikuwa anajiendeleza kawaida. Hakuwahi kuzungumza nami kuhusu mahusiano hayo. Nimekuwa nikijiuliza mbona. Labda kuna kitu ambacho hakutaka nijue ama kuna mambo ambayo yalikuwa yanamzuia kuniambia. Hayo ni kitendawili kwangu," Alisema.

Nduta ametoa wito kwa serikali kumsaidia kupata haki ya binti yake ambaye amemtaja kuwa mwerevu na asiye na hatia.