Tahadhari unazopaswa kuzingatia ili kulinda maisha yako unapoogelea

Miongoni mwa watu waliokufa maji hivi karibuni ni mtoto wa Davido.

Image: BBC

Mara kwa mara tumekuwa tukisia taarifa za watu kufa maji wanapokuwa wakiogelea. Miongoni mwa watu hao ni watoto ambao wamekuwa wakiambatana na wazazi au walezi wao kwenye vindimbwi vya kuogelea, baharini au wawapo nyumba.  

Miongoni mwa watu waliokufa maji  hivi karibuni ni mtoto wa muimbaji nyota wa Afrobeats Davido Ifeanyi Adeleke, ambaye alitimiza umri miaka mitatu mwezi uliopita, alikufa maji siku ya Jumatatu.

Lakini je unawezaje kuepuka ajali zinazotokea wakati mtu anapoogelea katika vidimbwi na maeneo mengine yenye maji?.

Akizungumza na BBC Mwalimu wa kuogelea kutoka Tanzania Alfred  Stanley Mlita, anasema mambo mbali mbali ya kimsingi yanapaswa kuzingatia  kuhusu kuogelea kwenye vidimbwi vya kuogelea (Swimming pool), mitoni, baharini, na maeneo mengine yenye maji. Amesisitiza kuwa wazazi na walezi wanajukumu kubwa la kuwachunga watoto wao wawapo katika maeneo ya kuogelea ili kuepuka ajali zinazotokea katika maeneo hayo ambazo zimekuwa zikisababisha vifo.

Usiwahi kamwe kuogelea peke yako : Kila mara hakikisha kuna mtu anayekutizama  wakati unapoogelea, ili aweze kukusaidia unapoogelea. Hata watu wazima. ‘’Hupaswi kwenda peke yako kuogelewa, iwe vidimbwini, kwenye fukwe za bahari  au maene mengine ya kuogelea…lazima mwende watu wawili au watatu kuogelea, unaweza kupoteza maisha wakati hakuna mtu wa kukuokoa, ukafa peke yako’’ anasema  Bw Mlita, ambaye ni mwalimu wa kuogelea jijini Dar es Salaam.

Ogelea na boya la uokozi- Life Jacket:   Vaa boya la uokozi wakati unapokwenda kuogelea ufukweni mwa bahari, au iuchukue boya  maalumu la kuogelea linaloweza kuelea ipasavyo unapoogelea kwenye kidimbwi (Swimming pool), yanaweza kukusaidia kuokoa maisha. Bw Mliti hata hivyo anatoa ushauri kwa wazazi  kuwaangalia wakati wowote watoto wao wanapoogelea hata wanapokuwa wamevalishwa maboya kwani ajali inaweza kutokea hata kama mtoto amevalishwa boya, anasema.

Chunguza kidimbwi (Swimming pool) kabla ya kuogelea : Je kina uzio na lango linaloweza kufungwa wakati wote?  Kifuniko cha kidimbwi - kinachoweza kuhimili uzito? Iwapo vitu hivyo havipo, watoto au Wanyama wanaweza kudumbukia kwa urahisi ndani ya kidimbwi cha kuogelea na kuzama .  Je kuna msimamizi au mtu anayeweza kuokoa maisha, wanasisitiza wataalamu mbali mbali wa uogeleaji wa vidimbwini( Swimming pools).

Zingatia usalama wa dimbwi la kuogelea la nyumbani:  Alfred  Stanley Mlita  anatoa ushauri kwa watu wenye vidimbwi vya kuogelea vya nyumbani kuwa makini hususan kwa usalama wa watoto: ‘’Unapokuwa na kidimbwi cha kuogelea nyumbani hakikisha mlango wa kuelekea kwenye dimbwi la kuogelea unafungwa wakati wote na hakikisha ufunguo wake unahifadhiwa mahala ambapo watoto wanaweza kuufikia, kwani watoto wanaweza kuingia dimbwini bila usimamizi wa mtu mzima na kuzama dimbwini peke yao’’

Aidha anasema wazazi na walezi wanapaswa  kufunika maji, yanayowekwa kwenye ndoo, matanki, karai na vifaa vingine kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, ili kuwaepusha watoto kutumbukia ndai ya vifaa hivyo na kufa maji.

Usiwahi kupiga mbizi katika maji yenye kina kifupi: Muulize msimamizi wa kidimbwi anayefahamu kuogelea au mzazi iwapo ni salama kupiga mbizi kwenye kidimbwi kabla ya kuogelea. Usipige mbizi kama hakuna mtu wa kumuuliza kuhusu usalama wa kidimbwi.’’ Ni hatari kupiga mbizi bila kujua kina cha maji, anasema Alfred  Stanley Mlita unaweza kujitupa kwenye kina kifupi kwa nguvu na kupasuka kichwa, kwahiyo usijaribu kuogelea kwenye maji ya kina ambacho haujui urefu wake ni hatari’’, anasisitiza

Jifunze kunusuru maisha ama kutoa huduma ya kwanza : Wazazi  & walezi wanapaswa kujifunza kutoa huduma ya kwanza hususan kwa watoto. ‘’Wazazi wanapaswa kujua kuwa jukumu la kulinda usalama wa watoto kwenye maeneo ya vidimbwi ni lao kwanza kuliko mtu yeyote mwingine yule…wazazi na walezi wanatakiwa kuhakikisha watoto hawakimbii maeneo yam aji kwani wanaweza kuteleza na kuvunjika au kuzama majini’’, anasema Bw Mliti.

Kila mara  unapokwenda kuogelea unashauriwa uache simu yako wazi, usiizime ili iweze kutumiwa wakati dharura inapotokea.

Hatahivyo unashauriwa “Usijaribu kujitupa ndani ya kidimbwi kuokoa!” : Mara kwa mara huu umekuwa ni ushauri unaotolewa katika maeneo mengi ya kuogelewa…Usiwahi kamwe kujaribu  kujitupa ndani ya kidimbwi kujaribu kumuokoa mtu yeyote, vinginevyo maisha ya watu wawili yatakuwa hatarini. Unaweza kusaidia kuokoa maisha ya mtu anayekaribia kuzama kwa kumtupia kitu kinachoelea, mfano Kamba ili ajisaidie mwenyewe kujiokoa.  Unaweza pia kupiga mayowe kuomba usaidizi.  

 Hakikisha kwamba maji ni salama: Je maji yako wazi? Unaweza kuitazama  chini kwenye sakafu ya kidimbwi? Je kuna mhusika anayeweza kuwajibika iwapo kutatokea dharura?

Jifunze kuogelea: Ni vyema kujifunza kuogelea mapema ili kupunguza hatari zitokanazo na kuogelea. Wataalamuwa kuogelea wanashauri katika umri wa miezi sita, watoto wanapaswa masomo ya kuogelea . Na watu wazima ambao hawafahamu kuogelea wanapaswa kujifunza kuogelea 

Heshimu miongonozo /sheria za vidimbwi vya kuogelea na usalama wa majini : Bw Mliti anasema haupaswi  kukimbia katika mazingira ya kidimbwi, kula ndani au kutafuna gum( mfano Big G) , au kubeba vifaa vyovyote ndani ya kidimbwi, kwani vinaweza kuhatarisha maisha. Kama hakuna msimamizi au muongozaji wa kuogelea mtu mzima, subiri kwanza hadi baadaye, usiogelee.