Siasa safi! Sakaja na Igathe hatimaye wakutana baada ya kuchuana vikali Nairobi

Sakaja alishinda ugavana baada ya kuzoa kura 699,392 huku Igathe akipata kura 573,518.

Muhtasari

•Sakaja alikutana na aliyekuwa mpinzani wake mkuu katika kinyang'anyiro cha kuwania kiti hicho cha juu zaidi katika kaunti, Polycarp Igathe.

•Hapo awali,Sakaja alitoa mwaliko wa kahawa kwa mgombea huyo wa Jubilee baada ya kukubali kushindwa 

wakati wa mkutano mnamo Agosti 18,2022.
Gavana Mteule wa Nairobi Johnson Sakaja na Polycarp Igathe wakati wa mkutano mnamo Agosti 18,2022.
Image: TWITTER// JOHNSON SAKAJA

Alhamisi, gavana mteule wa Nairobi Johnson Sakaja alikutana na aliyekuwa mpinzani wake mkuu katika kinyang'anyiro cha kuwania kiti hicho cha juu zaidi katika kaunti, Polycarp Igathe.

Sakaja alizamia kwenye mtandao wa Twitter kufichua habari kuhusu mkutano huo. Seneta huyo anayeondoka hata hivyo hakutoa maelezo mengi kuhusu mada ya mkutano hwao.

"Mazungumzo mazuri na kucheka na kaka yangu Polycarp Igathe mchana huu. Amesema ni #Naitunavyoitaka #SiasaSafi," Sakaja alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Hapo awali,Sakaja alitoa mwaliko wa kahawa kwa mgombea huyo wa Jubilee baada ya kukubali kushindwa katika uchaguzi wa Agosti 9.

 "Asante, Bwana. Ulikuwa mpinzani anayestahili na mfano halisi wa Siasa Safi. Hebu tunywe kahawa hivi karibuni," Alisema kupitia Twitter.

Seneta huyo anayeondoka alinyakua nafasi ya bosi wa kaunti  baada ya kupata kura 699,392.  Aliwania kwa tiketi ya UDA.

Igathe ambaye alikuwa mpinzani wa karibu wa Sakaja aliibuka katika nafasi ya pili baada ya kuzoa kura 573,518. 

Mgombea huyo wa Jubilee alimpongeza Sakaja kwa ushindi na kumtakia kila la kheri katika safari yake ya kuwatumikia wana Nairobi.

“Ninakubali uamuzi wa watu wa Nairobi na kuwashukuru wafuasi wetu wote. Gavana wa Nairobi ni Mheshimiwa Johnson Sakaja. Hongera! Mungu ibariki Kenya,” Igathe aliandika kwenye Twitter..

Siku ya Jumatano, Sakaja alisema atashirikiana na viongozi wote bila kujali itikadi zao ili kuboresha jiji.

"Kipindi cha kampeni kimekamilika na sasa mimi ndiye gavana wa Nairobi. Kazi yangu ni kuwatumikia wote na kujenga timu inayohudumia watu wetu. Tuliweka ahadi na lazima tutimize," Sakaja alisema.