Mpenzi wa zamani wa mwanafunzi aliyeuawa wa KMTC akamatwa

Muhtasari
  • Mpenzi wa zamani wa mwanafunzi aliyeuawa wa KMTC akamatwa
Mwanafunzi wa KMTC Homabay aliyeuawa Emily Chepkemoi
Image: Robert Omollo

Mpenzi wa zamani wa mwanafunzi wa Chuo cha kufundisha masomo ya udaktari mjini Homabay (KMTC-Homabay Town) ambaye aliuawa katika hosteli yake ya Homa Bay amekamatwa

Eli Odoyo, 37, alikamatwa Jumanne asubuhi kuhojiwa kwa ajili ya mauaji ya Emily Chepkemoi yaliyotokea Ijumaa iliyopita.

Afisa wa Kurugenzi ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai ya mji wa Homa Bay Monica Berege alisema mshukiwa ana uwezekano wa kuwa na habari muhimu juu ya mauaji hayo.

Berege alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.

KUlinagana na upasuaji wa mwili uliofanywa Siku ya Jumanne, mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 23 alikufa kutokana na kukosa hewa na alikuwa amedungwa  kisu mara tatu kichwani na mkono wa juu.

Mwili wa Emily Chepkemoi, 23, ulipatikana juu ya kitanda kilichokuwa ndani ya hosteli yake huku umezingirwa na dimbwi la damu.

Ndugu yake Joseph Kipruto ametaka haki.

"Sisi ni yatima kabisa katika familia yetu. Inasikitisha sana kwa kweli na tunachotaka ni haki, "alisema.

Kipruto aliongea walipopeleka mwili kwa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Msamaria huko Kapsabet, kaunti ya Nandi.

Wanafunzi wa KMTC waliwahimiza polisi kuharakisha uchunguzi na kutoa haki kwa wenzao.

Kiongozi wa muungano wa wanafunzi katika chuo hicho, David Odhiambo aliagiza haki kutendeka na akaomba uchunguzi kamilifu kufanyika.

Walisema kuwa haki ya haraka itazuia kurudiwa kwa tukio kama hilo chuoni.

"DCI inapaswa kuchunguza suala hilo na kumleta mtuhumiwa. Hawapaswi kusitisha uchunguzi wao hadi washukiwa wakamatwe, ”Odhiambo alisema.

Mwanafunzi mwenzake wa Chepkemoi Michele Akinyi alisema mauaji hayo ni hasara kubwa kwa udugu mzima wa chuo.

Alikuwa mnyenyekevu na mwenye kutia moyo kwa wengi wetu, kwa sababu ya bidii yake na kujitolea. Tutamkosa dada yangu mpendwa, "Akinyi alisema.