Watatu wapoteza maisha kufuatia mashambulizi yanayotuhumiwa kutekelezwa na Al-Shabaab, Mandera

Watu wengine wawili wanaripotiwa kunusurika na majeraha kufuatia mashambulizi hayo

Muhtasari

•Watu watatu katika kaunti ya Mandera walipoteza maisha yao wikendi iliyokamilika kwenye mashambulizi mawili tofauti ya kigaidi ambayo yanatuhumiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Al-Shabaab.

•Kulingana na polisi, mwanamke mgonjwa aliyekuwa anapelekwa hospitalini alikufa kutokana na shambulio hilo huku wengine wawili wakiugua majeraha.

Gari lililoshambuliwa Mandera
Gari lililoshambuliwa Mandera
Image: HISANI

Watu watatu katika kaunti ya Mandera walipoteza maisha yao wikendi iliyokamilika kwenye mashambulizi mawili tofauti ya kigaidi ambayo yanatuhumiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Al-Shabaab.

Watu wengine wawili wanaripotiwa kunusurika na majeraha kufuatia mashambulizi hayo.

Polisi walisema kuwa kwenye tukio la kwanza lililofanyika siku ya Jumamosi, magaidi walishambulia kwa risasi watu watatu waliokuwa wanasafiri kwa gari ndogo aina ya Saloon katika maeneo ya Kamor Bahaw kisha kutoroka.

Kulingana na polisi, mwanamke mgonjwa aliyekuwa anapelekwa hospitalini alikufa kutokana na shambulio hilo huku wengine wawili wakiugua majeraha.

Rukia Adan, 50, anaripotiwa kufa papo hapo wakati mwanawe Abdikadir Kuno, 35, alipatwa na risasi kwenye paja lake.

Masaa kadhaa baadae magaidi hao walishambulia gari lingine kwa risasi nje ya mji wa Fino  na kuua mwanaume mmoja na mwanawe papo hapo.

Polisi walisema kuwa Moulid Billow na Ahmed Bata walipoteza maisha yao baada ya gari walilokuwa wakisafiri nalo kumiminiwa risasi  na wanaodhaniwa kuwa wanamgambo wa Al-Shabaab.

Bosi wa polisi eneo la Kaskazini Mashariki, Rono Bunei amesema kuwa usalama umewekwa katika maeneo hayo huku polisi wakiendelea kuwatafuta washukiwa.