Mtoto wa miaka 5 apigwa na babake hadi kufa kwa kukosa kufanya kazi za nyumbani Nyamira

Mkewe mshukiwa alijaribu kumueleza kuwa mtoto wao hakuwa amehitimu umri wa kufanya kazi zozote pale nyumbani ila juhudi zake ziliangulia patupu kwaniOsoro alisisitiza kuwa mwanawe alifaa kupokea kichapo.

Muhtasari

•Kemunto alisema kuwa bwanake alikataa kumskiza na badala yake akamgeukia na kuanza  kumpiga mateke na ngumi. Hapo ndipo akaamua kupiga nduru ili kuomba usaidizi kutoka kwa majirani.

•Mtoto yule ambaye alikuwa analia kwa uchungu alipelekwa kitandani ili atulize machungu ila saa moja baadaye akapatikana akiwa ashakata roho.

crime
crime

Habari na Magati Obebo

Mwanaume mmoja kutoka maeneo ya Kitutu-Masaba, Nyamira alikamatwa kwa madai ya kupiga  mwanawe wa miaka mitano hadi akaaga.

Denis Osoro anaripotiwa kufika nyumbani kwake mwendo wa saa tatu usiku wa Jumamosi akiwa mlevi chakari na akaanza kudai kujua kazi ambazo mwanawe alishinda akifanya siku hiyo.

Mkewe mshukiwa, Violet Kemunto alijaribu kumueleza kuwa  mtoto wao hakuwa amehitimu umri wa kufanya kazi zozote pale nyumbani ila juhudi zake ziliangulia patupu kwani Osoro alisisitiza kuwa mwanawe alifaa kupokea kichapo.

Kemunto alisema kuwa bwanake alikataa kumskiza na badala yake akamgeukia na kuanza  kumpiga mateke na ngumi. Hapo ndipo akaamua kupiga nduru ili kuomba usaidizi kutoka kwa majirani.

Mtoto yule ambaye alikuwa analia kwa uchungu alipelekwa kitandani ili atulize machungu ila saa moja baadaye akapatikana akiwa ashakata roho.

Nyanya ya marehemu alidai kuwa walimpata akiwa ashafariki na hapo kilio kikubwa kilichoita majirani kikaanza. Alisema kuwa mwili wa mtoto huyo ulikuwa na majeraha mgongoni.