Kura za eneo la Mt Kenya zitakuwa za Raila Odinga- Peter Kenneth ahakikishia kinara wa ODM

Kenneth alisema kuwa ana uhakika kuwa wakati Raila ataanza kufanya kampeni maeneo hayo watu watabadili mawazo yao na kukubali kumpigia kura.

Muhtasari

•Kenneth amewakosoa wanaosema kuwa aliyekuwa waziri mkuu hawezi kujinyakulia kura kutoka eneo la Mt Kenya na kusema kuwa hayo ni maoni yao binafsi.

•Kenneth alisema kuwa janga la Korona ndilo lilikuwa imemzuia kinara wa ODM kuanza kujipigia debe katika eneo la Mlima Kenya.

PK
PK

Aliyekuwa mgombea kiti cha urais mwaka wa 2013 na ambaye alikuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth amepuuzilia mbali madai kuwa kinara wa ODM Raila Odinga hawezi kupigiwa kura na wakazi jamii ya GEMA.

Akizungumza kwenye mkutano kati ya viongozi wa kisiasa na wafanyibiashara kutoka eneo la mlima Kenya katika  eneo la Tigoni kaunti ya Kiambu siku ya Alhamisi, Kenneth aliwakosoa wanaosema kuwa aliyekuwa waziri mkuu hawezi kujinyakulia kura kutoka eneo la Mt Kenya na kusema kuwa hayo ni maoni yao binafsi.

Kenneth amewasihi viongozi wanaoeneza madai hayo kutozungumza kwa niaba ya jamii yote ya GEMA.

"Wale ambao wanasema kuwa mheshiwa Raila Odinga hawezi kupata kura  kutoka mlima Kenya, wanaongea kwa niaba ya nani? Hata hajakuja kuomba kura. Atakuja, atakuja hata na ndugu yake (Uhuru Kenyatta). Nasema vile ifaavyo, wacha watu wasiongee kwa niaba ya wengine." Kenneth alisema.

Mwanasiasa huyo ambaye aliwania kiti cha ugavana jijini Nairobi aliwasihi wafanyibiashara ambao walikuwa wamejumuika pale kumsaidia Raila kutafuta kura atakapozindua kampeni zake katika eneo la mlima Kenya.

"Tuache mgombea kiti wetu aje atuongeleshe, atushawishi na mwende mkaombe kura kwa niaba yake.. Mheshimiwa Raila ukija, tuma hawa watu waende mashinani wakutafutie kura na wakualike" Alisema Kenneth.

Kenneth alisema kuwa janga la Korona ndilo lilikuwa imemzuia kinara wa ODM kuanza kujipigia debe katika eneo la Mlima Kenya.

Alisema kuwa ana uhakika kuwa wakati Raila ataanza kufanya kampeni maeneo hayo watu watabadili mawazo yao na kukubali kumpigia kura.

"Niko na uhakika tukianza hii safari na tupige hatua watu watabadilisha maoni yao. Niko na uhakika kuwa kura za mlima Kenya zitakuwa za mheshimiwa Raila Odinga" Kenneth alisema.

Kwa kipindi cha miaka mingi wakazi wa eneo la kati wamemfanya aliyekuwa waziri mkuu kuwa adui wao nambari moja kisiasa.

Raila anatazamia kubadilisha mawazo ya asilimia kubwa ya jamii ya GEMA kufikia mwaka ujao ili aweze kuvuna kura zao ambazo zinadaiwa kuwa nyingi zaidi nchini.