Utata waibuka kuhusu tukio la risasi lililoripotiwa na mwanablogu Dennis Itumbi

Kamanda wa polisi maeneo ya Kasarani Peter Mwanzo alisema kuwa hawakupata ushahidi wowote katika eneo la tukio na hawawezi kuthibitisha kuwa kulikuwa na risasi zilizopigwa.

Muhtasari

•Itumbi anadai kuwa alikuwa anaendesha gari lake aina ya Mercedes Benz katika maeneo ya Garden Estate wakati gari lingine lilikuja mbele yake na kumzuia kusonga mbele.

•Kulingana na ripoti hiyo, Itumbi alipatwa na hisia kuwa jambo lile sio la kawaida na kuna kitu kibaya kilikuwa kinaendelea.

•Maafisa wa polisi walifika mahali Itumbi allikuwa na kumpata akiwa salama. Hata hivyo inadaiwa kuwa upande wa mbele wa gari lake ulikuwa umebondeka kidogo

Gari la Itumbi
Gari la Itumbi
Image: HISANI

Mida ya saa tano usiku wa Ijumaa mwanablogu Dennis Itumbi alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Kasarani kuhusiana na tukio linalodaiwa kuwa 'jaribio la mauaji'.

Kulingana na ripoti iliyoonwa na Radio Jambo, Itumbi anadai kuwa alikuwa anaendesha gari lake aina ya Mercedes Benz katika maeneo ya Garden Estate wakati gari lingine lilikuja mbele yake na kumzuia kusonga mbele.

"Iliripotiwa na Dennis Itumbi kuwa alikuwa anaendesha gari nambari KBU 285F aina ya Mercedes Benz katika barabara ya Garden Estate- Mountain Mall akielekea katika hoteli ya Red Sports kuchukua chajio wakati gari lake lilizuiliwa na gari lingine ambalo halijatambulishwa" Ripoti hiyo ilisoma.

Kulingana na ripoti hiyo, Itumbi alipatwa na hisia kuwa jambo lile sio la kawaida na kuna kitu kibaya kilikuwa kinaendelea.

"Alipatwa na shaka  na akaamua kugonga gari lile  ili apate nafasi ya kutoroka mbio." Ripoti hiyo ilisoma.

Inadaiwa kuwa alipokuwa anajaribu kutoroka aliskia milio ya risasi zilizokuwa zinaelekezwa kwa gari lake.

"Aliweza kutoroka mbio bila kuumia. Baadae aliegesha gari lake katika kituo cha petroli ca Rubis na kujulisha familia yake na polisi" Ripoti ilisema.

Maafisa wa polisi walifika mahali Itumbi allikuwa na kumpata akiwa salama. Hata hivyo inadaiwa kuwa upande wa mbele wa gari lake ulikuwa umebondeka kidogo.

 Hata hivyo, wakazi wa eneo ambalo tukio hilo linadaiwa kutokea wamesema kuwa hawakuskia milio ya risasi.

Kamanda wa polisi maeneo ya Kasarani Peter Mwanzo alisema kuwa hawakupata ushahidi wowote katika eneo la tukio na hawawezi kuthibitisha kuwa kulikuwa na risasi zilizopigwa.

Inaripotiwa kuwa hakuna risasi yoyote iliyotumika ilipatikana katika eneo la tukio.  Gari la Itumbi lilipelekwa katika kituo cha polisi cha Kasarani huku upelelezi ukiendelea.

Kamanda Mwanzo amesihi watu kuwa watulivu na kuwaonya dhidi ya kulifanya tukio hilo kuwa suala kubwa kwani uchunguzi wa polisi bado unaendelea.

Baadhi ya wanasiasa wanaomuunga mkono naibu rais William Ruto wakiongozwa na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi wamejitokeza kukashifu tukio hilo.