Hofu Kirinyaga baada ya mtoto wa miaka 4 kunajisiwa kisha kuuliwa, mshukiwa mkuu akamatwa

Mwili wa mtoto huyo wa darasa la chekechea ulipatikana kichakani siku ya Jumatano ukiwa na ishara za kubakwa.

Muhtasari

•Muchiri anadaiwa kuwasihi watoto hao kumpeleka kwake nyumbani akachukue kitu fulani ila ni msichana mhasiriwa tu aliyekubali kumfuata.

•Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika mochari ya Kibugi huku uchunguzi zaidi ukiendelea kufanywa.

Watoto wa shule
Watoto wa shule
Image: MAKTABA

Polisi katika kaunti ya Kianyaga wanamzuilia mwanaume mmoja anayetuhumiwa kunajisi na baadae kuua mtoto wa miaka minne.

Peter Muchiri, 38, alikamatwa baada ya polisi kufahamishwa na wakazi wa Kianyaga kuwa yeye ndiye mshukiwa mkuu

Kulingana na naibu bosi wa polisi katika eneo la Kirinyaga Mashariki Patrick Nyaang, Muchiri anatuhumiwa kuvizia msichana huyo mdogo alipokuwa anatoka shule siku ya Jumatatu  akiwa ameandamana na wanafunzi wenzake.

Muchiri anadaiwa kuwasihi watoto hao kumpeleka kwake nyumbani akachukue kitu fulani ila ni msichana mhasiriwa tu aliyekubali kumfuata.

Mwili wa mtoto huyo wa darasa la chekechea ulipatikana kichakani siku ya Jumatano ukiwa na ishara za kubakwa.

Nyaanga alisema kuwa mshukiwa alikamatwa wakati maafisa wa polisi walikuwa wameenda kufariji familia .

Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika mochari ya Kibugi huku uchunguzi zaidi ukiendelea kufanywa.

Wazazi wameagizwa kuwafuatilia watoto wao kwa karibu ili kuwalinda kutoka kwa watu wasio na maadili.

"Hata kama hakuna  kinachohalalisha kifo cha msichana huyo, wazazi wafunze watoto wao kutokubali zawadi na vitu vingine vya kupendeza kutoka kwa watu wasiojua kwani inahatarisha maisha yao" Nyaanga alisema.

Nyaanga aliwasihi wazazi kuwafunza watoto wao miongozo ya kimsingi na kanuni zitakazowaepusha kutokana na tukio kama lile.