Familia na waendesha pikipiki waandamana kudai haki ya vijana wanne waliouliwa Kitengela

Ombi kuu la waandamanaji hao lilikuwa haki itendeke na waliotekeleza mauaji yale watiwe mbaroni.

Muhtasari

•Kikundi hicho ambacho kiliandamana na baadhi ya wanafamilia wa vijana wanne walioangamia kilifululiza moja kwa moja hadi kituo cha polisi cha Kitengela kikidai kupata majibu kuhusiana na mkasa huo.

•Alipokuwa anahutubia waandamanaji waliokuwa wamejumuika, kiongozi wa chama hicho Sammy Kiumbe alilaani mauji dhidi ya waendesha pikipiki wa kibinafsi na kusema kuwa hawakuweza kupata majibu kamili kuhusu uchunguzi unaoendelea kwani bosi wa polisi katika kituo cha Kitengela hakuwepo.

Mike George 29, Fredrick Mureithi 22, Victor Mwangi 26, Nicholas Musa 28 na pikipiki zao zilizochomwa Kitengela
Mike George 29, Fredrick Mureithi 22, Victor Mwangi 26, Nicholas Musa 28 na pikipiki zao zilizochomwa Kitengela
Image: KURGAT MARINDANY

Siku ya Jumapili mamia ya waendesha pikipiki waliandamana kutoka jijini hadi Kitengela kulalamikia mauaji ya vijana wanne waliopoteza maisha yao mikononi mwa wafugaji waliowashuku kuwa wezi wa mifugo usiku wa Jumapili, Agosti 8.

Kikundi hicho ambacho kiliandamana na baadhi ya wanafamilia wa vijana wanne walioangamia kilifululiza moja kwa moja hadi kituo cha polisi cha Kitengela kikidai kupata majibu kuhusiana na mkasa huo.

Wakiwa wamebeba mabango makubwa yenye picha za vijana waliouliwa na kuandikwa jumbe za kulaani mauaji ya kiholela kutokana na mitindo ya maisha ya watu, wanachama wa  chama cha waendesha bodaboda waliandamana katika barabara ya Mombasa na ile ya kuelekea Kitengela wakiomboleza wenzao.

Ombi kuu la waandamanaji hao lilikuwa haki itendeke na waliotekeleza mauaji yale watiwe mbaroni.

Alipokuwa anahutubia waandamanaji waliokuwa wamejumuika, kiongozi wa chama hicho Sammy Kiumbe alilaani mauji dhidi ya waendesha pikipiki wa kibinafsi na kusema kuwa hawakuweza kupata majibu kamili kuhusu uchunguzi unaoendelea kwani bosi wa polisi katika kituo cha Kitengela hakuwepo.

"Hatutakubali kuendelea kuuliwa na ndio sababu tumekuja hapa leo pamoja na familia kuskia kuhusu hiyo kesi hiyo inaendeleaje. Vijana wamepelekwa kwenye eneo la tukio na polisi wanafanya kazi yao. Tulikuwa tumekuja kuambiwa vile kesi inaendelea lakini tumeambiwa kuwa OCPD ako Isinya na siku ya leo sio siku tungeweza kumuona. Tumeembiwa kuwa hatukuwa tumewaarifu sababu hakuwa kazini na hakuna mtu mwingine ambaye ana cheo ndogo ambaye anaweza kumwakilisha OCPD" Kiumbe alisema.

James Onduso ambaye ni ndugu ya mmoja wa waliouliwa, Mike Onduso, na ambaye alionekaa kajawa na hisia za majonzi aliomboleza kifo cha ndugu yake na kueleza kutoridhishwa kwake na namna kesi hiyo inaoendelea.

"Hakuna mtu wamekamata. Tumeenda na wao katika eneo la tukio kama mara nne kufikia sasa na hakuna kitu kimefanyika.. mtu asiwadanganye eti kuna haki. Hapo mahali wametufikisha hakuna haki wanatenda hapa" nduguye Mike ambaye alionekana kujawa na ghadhabu alisema.

Mike Ondusu atazikwa kwao Kisii siku ya Alhamisi nao  Fredrick Muriithi na ndugu yake Victor  Mwangi watazikwa maeneo ya Nyahururu siku ya Ijumaa ilhali Nicholas Musa atazikwa siku ya Jumamosi maeneo ya Ukambani.