Mshukiwa mkuu katika mauaji ya vijana wanne Kitengela azuiliwa kwa siku 10

Mshukiwa alienda mafichoni mjini Kitengela punde baada ya kupanga na kutekeleza mauaji yale takriban wiki moja iliyopita

Muhtasari

•Benson Melonyie Ole Mungai, 40, ambaye alikamatwa akiwa mafichoni mjini Kitengela mnamo Jumatatu jioni hata hivyo hakusomewa mashtaka kwani mahakama ilikubali ombi la upande wa mashtaka kukubalishwa kumzuilia mshukiwa kwa siku kumi ili kukamilisha uchunguzi.

Mike George 29, Fredrick Mureithi 22, Victor Mwangi 26, Nicholas Musa 28 na pikipiki zao zilizochomwa Kitengela
Mike George 29, Fredrick Mureithi 22, Victor Mwangi 26, Nicholas Musa 28 na pikipiki zao zilizochomwa Kitengela
Image: KURGAT MARINDANY

Mshukiwa mkuu katika mauaji ya vijana wanne waliopoteza maisha yao mnamo Agosti 8 maeneo ya Kitengela  alifikishwa mahakamani siku ya Jumanne.

Benson Melonyie Ole Mungai, 40, ambaye alikamatwa akiwa mafichoni mjini Kitengela mnamo Jumatatu jioni hata hivyo hakusomewa mashtaka kwani mahakama ilikubali ombi la upande wa mashtaka kukubalishwa kumzuilia mshukiwa kwa siku kumi ili kukamilisha uchunguzi.

Ole Mungai alihusishwa na mauji ya Fredrick Mureithi (30), ndugu yake mdogo Victor Mwangi (25), Mike George (29) na Nicholas Musa (28) baada ya uchunguzi wa Kisayansi kubainisha kuwa alikuwa katika eneo la tukio.

Wanne hao ambao walikuwa wamehudhuria sherehe ya kuadhimisha siku ya kuazaliwa ya jamaa wao waliuawa kwa kupigwa kitutu baada ya kudaiwa kuwa wezi wa mifugo.

Iliripotiwa kuwa mshukiwa alienda mafichoni mjini Kitengela punde baada ya kupanga na kutekeleza mauaji yale takriban wiki moja iliyopita.