Polisi akamatwa kwa kosa la kuibia dereva shilingi 1,100 kwa kutumia nguvu Murang'a

Baada ya dereva yule kukataa kutii agizo la kutoa hongo, polisi huyo anaripotiwa kunyakua shilingi 300 alizokuwa ameshika kwa mkono

Muhtasari

•Kulingana na DCI, polisi huyo alikamatwa baada ya dereva wa TukTuk kupiga ripoti kuhusu tukio hilo ambalo linadaiwa kufanyika mnamo Jumanne jioni.

•Polisi huyo kwa sasa anazuiliwa huku uchunguzi zaidi ukiendelea kufanyika ili kuhakikisha haki imetendeka.

Pingu
Image: Radio Jambo

Afisa mmoja wa polisi anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kabati, Murang'a kwa madai ya kumuibia dereva wa TukTuk shilingi 1,100.

Kulingana na DCI, polisi huyo alikamatwa baada ya dereva wa TukTuk kupiga ripoti kuhusu tukio hilo ambalo linadaiwa kufanyika mnamo Jumanne jioni.

Dereva huyo alisimulia jinsi polisi mshukiwa alisimamisha TukTuk yake na kumwagiza atoe hongo ya shilingi 2000.

Baada ya dereva yule kukataa kutii agizo la kutoa hongo, polisi huyo anaripotiwa kunyakua shilingi 300 alizokuwa ameshika kwa mkono.

Isitoshe, afisa huyo aliendelea kukagua mifuko ya jamaa huyo  na kupora kiasi cha shilingi 800 alizokuwa nazo, tukio lililoacha suruali ya mhasiriwa ikiwa imeraruka vipande vipande.

Dereva yule ambaye kwa wakati huo alikuwa amefadhaika alipiga ripoti kwa maafisa kutoka kituo cha Kabati ambao walikimbia katika eneo la tukio  kisha kumkamata afisa mhusika.

Polisi huyo kwa sasa anazuiliwa huku uchunguzi zaidi ukiendelea kufanyika ili kuhakikisha haki imetendeka.

Haya yanajiri huku polisi wengine wanne upande wa Ruiru wakiendelea kuzuiliwa kwa tuhuma za wizi wa mabavu walipokuwa katika harakati za kutekeleza mikakati iliyowekwa kudhibiti janga la Corona usiku wa Jumanne.

Makonstabo hao wanadaiwa kukamata jamaa mmoja mnamo Agosti 12 maeneo ya Ruiru kwa kukiuka sheria za kafyu kisha kumuibia.

 Mmoja wa maafisa hao alichukua simu ya jamaa huyo, akamwagiza amfichulie pini yake na kutuma shilingi 1,030 kwa namba nyingine.