Viongozi wa OKA wakanusha madai kwamba Uhuru aliwalazimisha kumuunga Raila mkono

Muhtasari
  • Viongozi wa OKA wakanusha madai kwamba Uhuru aliwalazimisha kumuunga Raila mkono
Image: PSCU

Wakuu wa Kenya Alliance, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Moses Wetangula na Gideon Moi wametupilia mbali ripoti kwamba wamekubali kumuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi wa urais mwakani.

Katika taarifa ya pamoja Alhamisi, wakuu wa OKA walisema kwamba wakati wa mkutano wao na Rais Uhuru Kenyatta, hakuna chochote kilichojadiliwa juu ya kuunga mkono mtu yeyote kwa ajili ya kuwania kiti cha urais.

"Hakuna mtu aliyeuliza au hata alipendekeza kwamba tumuunge mkono mtu yeyote kwa chochote," Mudavadi alisema.

Viongozi hao walisisitiza kwamba mkutano wao na Rais ulikuwa wa kujadili juu ya maswala ya masilahi ya kitaifa, kati yao hatua mpya zakuthibiti maambukizi ya covid-19.

Wakuu pia walishutumu vyombo vya habari na haswa Daily Nation kwa kile walichokiita kama "ripoti ya uwongo".

Gazeti la Daily Nation Alhamisi lilikuwa limechapisha habari kwenye kurasa zake za mbele zilizosomeka "Uhuru awalazimu machifu wa OKA kumuunga mkono Raila".

Wakuu hao walishutumu gazeti hilo kwa kutunga hadithi kwenye mikutano yao na Uhuru, kwa niaba ya mwalikwa mmoja (Raila Odinga).

"Wakenya wanastahili kuripoti sahihi, ya ukweli, inayothibitishwa, inayotokana na usawa na uratibu wa hafla na sio hadithi za uwongo juu ya hafla zilizotengenezwa ambazo hazikutokea; zilitakaswa kupitia sura ya ukweli wa ubunifu,ukweli wa udanganyifu, vyanzo visivyo na maana na mantiki iliyopotoka."

Vyama vya siasa vilifanya mkutano na Rais Uhuru Kenyatta Jumatano katika Ikulu ya Mombasa.

Taarifa ya Msemaji Kanze Dena ilisema viongozi ambao walijumuisha; Raila Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Gideon Moi (KANU) na Moses Wetangula (Ford Kenya), walikubaliana kuchukua jukumu kuu katika kuhamasisha Wakenya kutii sheria za Covid-19 na hatua ikiwa ni pamoja na kuchukua chanjo.