Faraja baada ya mwanafunzi aliyetekwa nyara akielekea nyumbani kwa likizo fupi kupatikana Embu

Waliomteka Nderi nyara walimlazimisha kuvua sare yake ya shule na wakampatia nguo za kawaida avalie.

Muhtasari

•Jacob Nderi, 16, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya upili ya Barnabas Kavengero alitupiwa blanketi na mtu aliyekuwa kwenye gari lililopita kando yake, akahisi uchungu kali mkononi na hakumbuki chochote kingine kilichotokea pale katika eneo la tukio.

•Rafiki mmoja wa familia, Tabitha Wanja ambaye alizungumza na mhasiriwa amesema kuwa Nderi alimwarifu kuwa alitekwa nyara na watu ambao hawafahamu waliokuwa wameabiri gari nyekundu.

Jane Muthoni na mwanawe Jacob Njeru siku ya Alhamisi, Agosti 26
Jane Muthoni na mwanawe Jacob Njeru siku ya Alhamisi, Agosti 26
Image: BENJAMIN NYAGAH

Habari na Benjamin Nyagah

Kijana mmoja kutoka Embu aliyetekwa nyara wakati alikuwa akielekea nyumbani kwa likizo fupi siku ya Jumapili amepatikana akiwa mwenye afya ila akionekana dhaifu.

Jacob Nderi, 16, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya upili ya Barnabas Kavengero alitupiwa blanketi na mtu aliyekuwa kwenye gari lililopita kando yake, akahisi uchungu kali mkononi na hakumbuki chochote kingine kilichotokea pale katika eneo la tukio.

Mama ya mhasiriwa amesema kuwa mwanawe alitekwa nyara mnamo Jumapili jioni na alipatikana siku ya Jumanne katika kijiji cha Karurumo kilicho karibu na mpaka wa Embu na Mbeere.

Alisema kuwa mwanzoni alidhani  mwanawe alikuwa ameamua kutazama mechi ya soka shuleni  kama ilivyokuwa kawaida yake ila akagundua kuwa kufikia mida ya saa kumi jioni ya Jumatatu Nderi hakuwa amerejea nyumbani.

Kufuatia hayo akapiga ripoti katika kituo cha polisi cha Siakago na hapo mikakati ya kutafuta mwanawe ikang'oa nanga.

Rafiki mmoja wa familia, Tabitha Wanja ambaye alizungumza na mhasiriwa amesema kuwa Nderi alimwarifu kuwa alitekwa nyara na watu ambao hawafahamu waliokuwa wameabiri gari nyekundu.

Wanja alisema kuwa waliomteka Nderi  nyara walimlazimisha kuvua sare yake ya shule na wakampatia nguo za kawaida avalie.

Mkoba wa Nderi pamoja na sare ya shule zilipatikana katika kijiji cha Mutitu Andei kilicho karibu na nyumbani kwao, Kavengero.

Siku ya Jumatano, wakazi wa kijiji cha Kavengero walishiriki maandamano wakitaka kupata majibu kuhusiana na kutoweka kwa kijana huyo.

Naibu kamanda wa kaunti ya Embu Lucy Ndemo amesema kuwa Nderi alipatikana mida ya saa moja usiku wa Jumatano na akapelekwa katika hospitali ya Siakago.

Polisi wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na kisa hicho huku  washukiwa kadhaa wakiwa wametiwa mbaroni tayari.