Takriban watu 500 wadaiwa kula kiapo kuficha majina ya waliohusika na mauaji ya vijana 4 Kitengela, wapelelezi wachunguza

Inaripotiwa kuwa wazee wa kijiji waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo walitishia kulaani yeyote ambaye angefichua waliohusika kwa maafisa wa polisi.

Muhtasari

•Wapelelezi wanachunguza ripoti kuwa zaidi ya watu 500 walikula kiapo maeneo ya Kitengela kuficha majina ya waliohusika katika mauaji ya vijana wanne wa familia moja mapema mwezi huu.

Mike George 29, Fredrick Mureithi 22, Victor Mwangi 26, Nicholas Musa 28 na pikipiki zao zilizochomwa Kitengela
Mike George 29, Fredrick Mureithi 22, Victor Mwangi 26, Nicholas Musa 28 na pikipiki zao zilizochomwa Kitengela
Image: KURGAT MARINDANY

Wapelelezi wanachunguza ripoti kuwa takriban watu 500 walikula kiapo maeneo ya Kitengela kuficha majina ya waliohusika katika mauaji ya vijana wanne wa familia moja mapema mwezi huu.

Mkutano huo unadaiwa kufanyika takriban wiki mbili zilizopita na inaripotiwa kuwa wazee wa kijiji waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo walitishia kulaani yeyote ambaye angefichua waliohusika kwa maafisa wa polisi.

Punde baada ya hafla hiyo kufanyika, mshukiwa mkuu kwenye mauaji ya vijana hao, Benson Melonyie Ole Mungai alikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Melonyie anaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kitengela  huku mahakama ikimuongeza siku nne zaidi za kuzuiliwa siku ya Ijumaa.

Hakimu Becky Cheloti aliamuru Melonyie azuiliwe katika kituo cha Kitengela hado tarehe 1 mwezi September ambapo kesi dhidi yake itaanza upya.

Upande wa mashtaka uliarifu mahakama kuwa kuna upelelezi zaidi unaoendelea na wanatazamia kuwasilisha washukiwa zaidi mahakamani.

Melonyie pamoja na wengine ambao hawakufikishwa mahakamani wanahusishwa na mauaji ya ndugu wawili Fredrick Mureithi(30) na Victor Mwangi (25), pamoja na Mike George(29) na Nicholas Musa (28)