Jamaa apigwa kitutu baada ya kutishia 'bouncer' na bastola bandia alipozuiwa kuingia kilabu Kajiado

Joshua Kalama anaripotiwa kushambuliwa na walinzi hao alfajiri ya Jumamosi alipotishia kumpiga risasi mlinzi wa kilabu cha Square aliyemzuia kuingia mle ndani kujiburudisha.

Muhtasari

•Kalama ambaye alikuwa amerauka macheo kuenda kujivinjari katika kilabu hiyo alisimamishwa langoni na kwa kughadhabishwa na hatua hiyo akatoa kifaa cha plastiki kilichofanana na bastola alichokuwa amesitiri kiunoni na kutisha kumpiga risasi mlinzi Cleophas Otieno aliyemzuia kuingia

Bouncer
Bouncer
Image: SHUTTER_STOCK

Jamaa mmoja mwenye umri wa miaka 29 anaendelea kupokea matibabu hospitalini baada ya kupigwa kitutu na walinzi wenye ghadhabu alipotishia mmoja wao na bastola bandia katika kiingilio cha kilabu moja mjini Kajiado.

Joshua Kalama anaripotiwa kushambuliwa na walinzi hao alfajiri ya Jumamosi alipotishia kumpiga risasi mlinzi wa kilabu cha Square aliyemzuia kuingia mle ndani kujiburudisha.

Kalama ambaye alikuwa amerauka macheo kuenda kujivinjari katika kilabu hiyo alisimamishwa langoni na kwa kughadhabishwa na hatua hiyo akatoa kifaa cha plastiki kilichofanana na bastola alichokuwa amesitiri kiunoni na kutisha kumpiga risasi mlinzi Cleophas Otieno aliyemzuia kuingia.

Otieno ambaye alikuwa kajawa na woga kwa wakati ule alikuwa karibu kumpisha Kalama apite ila akagundua kuwa 'bastola' ile haikuwa na uwezo wa kupiga risasi. Hapo akamuangusha Kalama sakafuni na kuitana.

Kikundi kikubwa cha walinzi wengine waliokuwa wamelinda mahali mbalimbali pale mjini kilifika kusaidia mmoja wao kumwadhibu Kalama.

Ngumi, mateke na vipigo vya aina zote vilishamiri pale na ilichukua kuwasili kwa maafisa wa polisi ili vita hivyo visitishwe la sivyo Kalama angepoteza maisha yake.

Hapo Kalama alikimbizwa hospitalini akiwa mwenye maumivu tele na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya wizi wa mabavu yanayomkabili.