Sina muda wa kujibizana na wapinzani wangu!- DP Ruto

Ruto alisema kuwa hana muda wa kujadili masuala ya vyeo, madaraka na ulinzi kwani tayari ako na kazi muhimu ya kuboresha uchumi.

Muhtasari

•Ruto alisema kuwa yu mbioni kutengeneza mfumo maalumu wa kiuchumi wa kuanzia chini kwenda juu maarufu kama Bottom up na anatafuta washirika watakaomsaidia kuboresha maisha ya Wakenya.

•Alisema kuwa ni muhimu viongozi waangazie namna ya kutengeza ajira kwa mamilioni ya Wakenya kabla ya kujadili masuala ya ugavi wa madaraka.

Ruto akihutubia waombolezaji katika mazishi ya seneta mteule Victor Prengei siku ya Jumamosi
Ruto akihutubia waombolezaji katika mazishi ya seneta mteule Victor Prengei siku ya Jumamosi
Image: DPPS

Naibu Rais William Ruto amesema kuwa hana muda wa kujibizana na wanasiasa wanaompinga na kumdharirisha kisiasa.

Alipokuwa anahutubia waombolezaji katika mazishi ya seneta mteule Victor Prengei katika eneo la Marioshoni, Njoro siku ya Jumamosi, Ruto alisema kuwa yu mbioni kutengeneza mfumo maalumu wa kiuchumi wa kuanzia chini kwenda juu maarufu kama Bottom up na anatafuta washirika watakaomsaidia kuboresha maisha ya Wakenya.

Naibu Rais alikuwa ameandamana na wabunge zaidi ya ishirini kutoka mrengo wa Tangatanga. Wengine ambao walihudhuria hafla hiyo ni pamoja na Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui , naibu wake Erick Korir na Spika wa Seneti Ken Lusaka.

Ruto alisema kuwa hana muda wa kujadili masuala ya vyeo, madaraka na ulinzi kwani tayari ako na kazi muhimu ya kuboresha uchumi.

"Pole sana kwa wale ambao walitaka tujadili masuala ya madaraka, vyeo na ulinzi. Mimi najishughulisha kutengeneza mfumo wa uchumi wa Bottom-Up ambao utahakikisha kuwa kazi zimepatikana, kuna uwezeshaji na wananchi wa kawaida wamepata ulinzi ili nchi yetu iweze kusonga mbele" Ruto alisema.

Mgombeaji huyo wa kiti cha urais mwaka ujao alisema kuwa ni muhimu viongozi waangazie namna ya kutengeza ajira kwa mamilioni ya Wakenya kabla ya kujadili masuala ya ugavi wa madaraka.

Alisema kuwa viongozi wanafaa kuwezesha raia wa kawaida ili waweze kujikimu kimaisha na kudai kuwa usalama wa raia wa kawaida unafaa kupewa kipaumbele.

" Naamini kuwa kabla tujadili masuala ya vyeo vyetu kama viongozi, ni lazima kwanza tuwe na mpango wa vile tutatengeneza ajira kwa mamilioni ya vijana nchini. Kabla tujadili namna tutagawana madaraka, ni lazima tuwe na mpango ya kuwezesha wafanyibiashara na wakulima wa kawaida ili tuweze kuwainua na kuhakikisha kuwa wamepata usaidizi wa kutosha kufanya vyema. Kabla ya kujadili usalama  wetu kama viongozi ni lazima kwanza tujadili usalama wa mwananchi wa kawaida. Hivo tu ndivyo tutaweza kuwa na taifa ambapo hakuna anayehisi ameachwa nyuma" Alisema Ruto.

Ruto aliahidi wakazi wa eneo hilo kwamba sasa Kazi ya mandeleo itaendelea baada ya 'reggae' kutupiliwa mbali.