Abiria 5 wapoteza maisha kufuatia ajali mbaya iliyotokea Kericho baada ya gurudumu la matatu kupasuka

Ajali hiyo ilitokea wakati gurudumu la matatu ambayo marehemu walikuwa wameabiri lilipasuka na kusababisha gari hilo kupoteza mwelekeo, likaanguka na kubingirika mara kadhaa

Muhtasari

•Abiria watatu waliaga papo hapo wakati wengine wawili walikata roho walipokuwa wanahudumiwa katika hospitali ya Londiani.

•Inaripotiwa kuwa matatu hiyo ambayo ilikuwa imekodishwa ilikuwa imebeba abiria 14 kutoka  Nakuru kuelekea Kisumu.

Mabaki ya matatu iliyoanguka
Mabaki ya matatu iliyoanguka
Image: HISANI

Habari na Sonu Tano

Watu watano walipoteza maisha yao kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea maeneo ya Londiani kaunti ya Kericho siku ya Jumapili.

Ajali hiyo ilitokea wakati gurudumu la matatu ambayo marehemu walikuwa wameabiri  lilipasuka na kusababisha gari hilo kupoteza mwelekeo, likaanguka na kubingirika mara kadhaa. Upande mmoja wa matatu hiyo ulikuwa umeharibika vipande vipande.

Abiria watatu waliaga papo hapo wakati wengine wawili walikata roho walipokuwa wanahudumiwa katika hospitali ya Londiani.

Waliohusika kwenye ajali hiyo iliyotokea kwenye barabara ya Kericho-Nakuru walikimbizwa hospitalini. Takriban abiria 9 ambao walinusurika kifo wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Londiani na inaripotiwa kuwa hali yao ni imara.

Miili ya abiria watano ambao walipoteza maisha yao ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Londiani.

Inaripotiwa kuwa matatu hiyo ambayo ilikuwa imekodishwa ilikuwa imebeba abiria 14 kutoka  Nakuru kuelekea Kisumu.

Kamishna wa maeneo ya Kipkelion Mashariki Elmi Ibrahim alisema kuwa guruduma moja la matatu hiyo lilipasuka na kuifanya ipoteze mwelekeo kisha ikaanguka na kubingirika mara kadhaa. Upande wa kushoto wa matatu hiyo ulikuwa umeharibiwa vipande vipande.