Kenya inahitaji kina Daudi ili kuondoa kina Goliathi madarakani - Jimi Wanjigi asema

Alisema kuwa uchumi wa nchi hauwezi fufuliwa na wanasiasa kama Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na William Ruto kwani wamekuwa serikalini kwa miaka mingi.

Muhtasari

•Wanjigi alisema kuwa wanaowania kiti cha urais nchini wamekuwa kwenye ulingo wa siasa kwa kipindi cha  zaidi ya miaka 30 na hawana chochote kipya cha kupea Wakenya.

•Wanjigi alisema kuwa changamoto zinazokabili nchi kwa sasa zinahitaji mtazamo tofauti ili kupata suluhu.

Jimi Wanjigi
Jimi Wanjigi
Image: EUTYCAS MUCHIRI

Mfanyibiashara na mwanasiasa mashuhuri  nchini Jimi Wanjigi amesema kuwa wakati umewadia wa Kenya kupata viongozi wapya.

Alipokuwa anahutubia waumini katika kanisa ya ST Peter ACK mjini Nyeri siku ya Jumapili, Wanjigi alisema kuwa wanaowania kiti cha urais nchini wamekuwa kwenye ulingo wa siasa kwa kipindi cha  zaidi ya miaka 30 na hawana chochote kipya cha kupea Wakenya.

"Ni wakati wa Daudi wengine wapya  nchini kusimama na kusema yametosha na kuwafagia (Goliathi) wote kutoka uongozini" Wanjigi alisema.

Alisema kuwa Kenya iko na 'Goliathi' wengi ambao wanafaa kuondolewa madarakani na viongozi wapya aliowaita 'Daudi'.

Bwenyenye huyo alisema kuwa uchumi wa nchi hauwezi fufuliwa na wanasiasa kama Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na William Ruto kwani wamekuwa serikalini kwa miaka mingi.

" Wao ndio kiini cha matatizo yanayokabili nchi kwa sasa. Ni Raila Odinga pekee ambaye tunaweza kuita shujaa wa ukombozi wa pili" Wanjigi alisema.

Hata hivyo alisema kuwa Raila alifanya jukumu lake wakati wa ukombozi wa pili ambapo alipigania haki za binadamu na  kwa sasa wakati wake umekwisha.

Wanjigi alisema kuwa changamoto zinazokabili nchi kwa sasa zinahitaji mtazamo tofauti ili kupata suluhu.

"Kenya inafaa kufungua ukurasa mpya mwaka wa 2022 na kuwa na viongozi wapya ambao watasaidia kwenye ukombozi wa tatu ambao ni wa kiuchumi"  Alisema Wanjigi.

Alisema kuwa ukombozi wa kwanza ulikuwa wakati wa kupigania uhuru ilhali wa pili ulikuwa wakati wa kupigania demokrasia ya vyama vingi.

(Utafsiri: Samuel Maina)