Afisa wa GSU aliyetishia kuua familia yake kwa bunduki akamatwa Mwingi

Bi Mutethya alinusurika baada ya bastola ile kuanguka wakati walikuwa wanaendelea kuzozana na mwanawe wa miaka 15 akaichukua kwa haraka sana.

Muhtasari

•Shadrack Munyao ambaye ni afisa wa GSU anayefanya kazi jijini Nairobi anaripotiwa kutoa bastola  yake na kuelekeza mtutu wake kwa mkewe Christine Mutethya pamoja na mwanawe walipokuwa wanazozana.

crime scene
crime scene

Habari na Kasera Onyango

Afisa mmoja anazuiliwa katika kituo cha polisi upande wa Mwingi kwa kutishia kumpiga mkewe risasi kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Shadrack Munyao ambaye ni afisa wa GSU anayefanya kazi jijini Nairobi anaripotiwa kutoa bastola  yake na kuelekeza mtutu wake kwa mkewe Christine Mutethya pamoja na mwanawe walipokuwa wanazozana.

Kulingana na naibu kamanda wa polisi maeneo ya Mwingi Peter Kaluma, bastola ya Munyao  kwa wakati huo ilikuwa na risasi 12.

Bi Mutethya alinusurika baada ya bastola ile kuanguka wakati walikuwa wanaendelea kuzozana na mwanawe wa miaka 15 akaichukua kwa haraka sana.

Punde baada ya hayo, Bi Mutethya pamoja na mwanawe waliandamana moja kwa moja hadi kituo cha polisi cha Mwingi Central ambapo walikabidhi maafisa wa polisi bastola waliyokuwa wamebeba kisha kuandikisha ripoti.

Munyao ambaye amekuwa katika kipindi cha likizo tangu Agosti 15 alifuata familia yake nyuma na alipokuwa pale katika kituo cha polisi akatiwa mbaroni ili ahojiwe na hatua zaidi ichukuliwe.