Mawakili wa washukiwa wa mauaji ya ndugu wawili wa Kianjokoma wajiondoa kwenye kesi

Muhtasari

•Washukiwa walitoa ombi kwa mahakama iwaruhusu watafute mawakili wengine kwani waliokuwa wanawawakilisha walikuwa wamejiondoa.

•Jaji Ogembo aliagiza naibu msajili wa mahakama kuwapatia mawakili wa serikali siku ya Jumatano na watasomewa mashtaka mnamo Alhamisi.

Maafisa sita ambao wamehusishwa na mauaji ya ndugu wawili Embu
Maafisa sita ambao wamehusishwa na mauaji ya ndugu wawili Embu
Image: ENOS TECHEE

Habari na Annette Wambulwa

Maafisa sita waliohusishwa na mauaji ya ndugu wawili kutoka Kianjokoma, Embu mwezi uliopita walikosa kusomewa mashtaka siku ya Jumanne na hatua hiyo kuahirishwa hadi siku nyingine.

Hii ilifuatia kujiondoa kwa mawakili waliokuwa wanawakilisha washtakiwa kwenye kesi ya mauaji inayowakabili.

Washukiwa walitoa ombi kwa mahakama iwaruhusu watafute mawakili wengine kwani waliokuwa wanawawakilisha walikuwa wamejiondoa.

Jaji Daniel Ogembo alisema kuwa ni muhimu washukiwa wale wawakilishwe na wakili na kusema kuwa hangeruhusu wazuiliwe Industrial Area kwani jambo hilo lingefanya iwe ngumu kwao kupata mawakili wapya.

Aliagiza naibu msajili wa mahakama kuwapatia mawakili wa serikali siku ya Jumatano na watasomewa mashtaka mnamo Alhamisi.

Ogembo alisema kuwa kila mmoja wao atapatiwa wakili na pia itakuwa sawa kwao kufika mahakamani ikiwa wataweza kupata wakili wenyewe. 

Washukiwa hao, Benson Mputhia, Consolata Kariuki, Nicholas Cheruiyot, Martin Wanyama, Lilian Chemuna na James Mwaniki kwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill.

Washukiwa tano pekee ndio walikuwa wamefika mahakamani kwani mmoja wao, Consolata Kariuki, alikuwa mgonjwa kulingana na wakili  Danstan Omari.