Walimu wakuu wachunguzwa kufuatia picha iliyoonyesha wanafunzi wakiwa wamefungwa kwenye mti kama adhabu

Muhtasari

•Picha ya wanafunzi watatu waliokuwa wamefungwa pamoja kwenye mti imeenea sana mitandaoni siku za hivi karibuni, kitendo ambacho kimelaaniwa sana na wanamitandao na kusemekana kuwa adhabu iliyokithiri.

Image: HISANI

Habari na KNA Nyandarua

Ofisi ya DCI imeagizwa kuanzisha uchunguzi dhidi ya waalimu wawili wakuu katika shule ya msingi ya Thiru iliyo eneo la Laikipia Magharibi kufuatia tukio moja ambapo watoto watatu walifungiliwa kwa mti kama adhabu.

Picha ya wanafunzi watatu waliokuwa wamefungwa pamoja kwenye mti imeenea sana mitandaoni siku za hivi karibuni, kitendo ambacho kimelaaniwa sana na wanamitandao na kusemekana kuwa adhabu iliyokithiri.

Kikosi cha kazi kilichoongozwa na naibu kamishna wa eneo la Nyahururu Moses Muroki kilifika katika shule hiyo asubuhi ya Jumatano na baadhi ya waalimu na wanafunzi wakaandikisha taarifa kuhusu tukio hilo.

Muroki aliagiza ofisi ya DCI kuanzisha uchunguzi dhidi ya mwalimu mkuu Shelmith Thimba na naibu wake David Maina ambao wanadaiwa kuadhibu wanafunzi hao kwa kuwafungilia kwenye mti iIjumaa iliyopita.

Naibu mwalimu mkuu anadaiwa kupiga picha ya wanafunzi hao wakiwa wamefungwa kwenye mti na kuituma kwenye kikundi cha waalimu cha WhatsApp kabla ya mwalimu mwingine kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Hatua kali itachukuliwa dhidi ya wakuu wa shule hiyo iwapo watapatikana na hatia.