Kijana wa miaka 19 anayedaiwa kupigwa risasi na polisi aaga dunia Kiamaiko

Risasi hiyo inaripotiwa kumpata kijana huyo tumboni.

Muhtasari

•Tukio hilo lilisababisha maandamano makubwa katika maeneo hayo ya Kiamaiko huku waandamanaji wakilalamikia unyama wa polisi

Crime scene
Crime scene

Kijana wa miaka 19 anadaiwa kuaga dunia baada ya kupatwa na risasi iliyopigwa hewani maeneo ya Kiamaiko kaunti ya Nairobi siku ya Alhamisi.

Inaripotiwa kuwa kijana huyo alikuwa amesimama kwenye roshani ya nyumba yao wakati mmoja wa maafisa ambao walikuwa wanafanya msako alipiga risasi hewani ili kufurusha kikundi cha wakazi ambacho kilikuwa kinalalamikia matumizi mabaya ya nguvu za polisi.

Risasi hiyo inaripotiwa kumpata kijana huyo tumboni.

Punde baada ya hayo kijana huyo alikimbizwa hospitalini ili kujaribu kuokoa maisha yake ila kwa bahati mbaya akapoteza maisha yake alipokuwa anapokea matibabu. 

Tukio hilo lilisababisha maandamano makubwa katika maeneo hayo ya Kiamaiko huku waandamanaji wakilalamikia unyama wa polisi.

Uchunguzi zaidi kuhusiana na ripoti hizo umeanzishwa huku mashahidi wote wakiagizwa kuandikisha taarifa katika kituo cha polisi.

Upasuaji wa mwili unatarajiwa kufanyika leo (Ijumaa) ili kubaini kilichosababisha kifo cha kijana huyo.