Mwanamke apiga mwanawe hadi kifo Kitengela, apiga ripoti kuwa mtoto alianguka kutoka kwa kiti ili kuficha ukweli

Muhtasari

•Akiwa na nia ya kuficha unyama aliokuwa ametendea mwanawe, Mercy Mwauli alifika katika kituo cha polisi cha Kitengela na kuarifu maafisa kuwa mtoto wake alikuwa ameanguka vibaya na kupata majeraha kichwani wakiwa nyumbani kwao.

•Baba ya marehemu, Dick Anjichi Ndubukhile ambaye alitilia matukio hayo shaka sana aliagiza upasuaji wa mwili ufanyike ili kubaini wazi kilichosababisha kifo cha mwanawe.

crime scene
crime scene

Polisi upande wa Kitengela wanamzuilia mwanamke mmoja aliyempiga mwanawe vibaya hadi akaaga kisha akapiga ripoti kuwa mwanawe alikuwa ameanguka kutoka kwa sofa.

Akiwa na nia ya kuficha unyama aliokuwa ametendea mwanawe, Mercy Mwauli alifika katika kituo cha polisi cha Kitengela mida ya saa moja unusu siku ya Jumatano na kuarifu maafisa kuwa mtoto wake , Dickens Anjichi alikuwa ameanguka vibaya na kupata majeraha kichwani wakiwa nyumbani kwao katika ghorofa ya Ngewa.

Mtoto huyo alikimbizwa katika hospitali  ya Shalom kwenye harakati ya kujaribu kunusuru maisha yake ila akangamia kutokana na majeraha mabaya alipokuwa anahudumiwa .

Kufuatia hayo, baba ya marehemu, Dick Anjichi Ndubukhile ambaye alitilia matukio hayo shaka sana aliagiza upasuaji wa mwili ufanyike ili kubaini wazi kilichosababisha kifo cha mwanawe.

Upasuaji wa mwili ambao ulishuhudiwa na wapelelezi pamoja na baba ya mtoto huyo uliashiria kuwa marehemu aliangamia kutokana na  majeraha mabaya kwenye viungo vyake ikiwemo mikononi, kichwani na kwenye mapaja.

Baada ya kupokea matokeo ya mwanapatholojia, wapelelezi walifululiza moja kwa moja hadi nyumbani kwa Bw Anjichi na kuhoji Bi Mwauli pamoja na msimamizi wa ploti hiyo.

Bi Mwauli alitiwa pingu baada ya kubainika kuwa  alimpiga mwanawe kuhusiana na jambo ambalo halijafahamika bado. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la mauaji.