Jamaa apiga mkewe hadi kifo baada ya kumpata akiwa amebugia chang'aa na kulewa chakari, Siaya

Muhtasari

•Kevin Onyango 34, anaripotiwa kumshambulia mkewe Emmaculate Mayavi 42, kwa mateke na mangumi baada ya kumpata kwa  baa moja inayouzwa chang'aa iliyo katika kijiji cha Jera eneo la Ugenya, kaunti ya Siaya.

crime scene
crime scene

Jamaa mmoja anazuiliwa katika kituo cha polisi kwa kupiga mkewe hadi kifo baada ya kumpata katika kibanda cha chang'aa akiwa mlevi chakari.

Kevin Onyango 34, anaripotiwa kumshambulia mkewe Emmaculate Mayavi 42, kwa mateke na mangumi baada ya kumpata kwa  baa moja inayouzwa chang'aa iliyo katika kijiji cha Jera eneo la Ugenya, kaunti ya Siaya.

Kulingana na DCI, Onyango alirejea nyumbani kwake mida ya jioni siku ya Jumamosi na kumkosa mkewe na hapo akapiga hatua ya kumtafuta.

Baada ya kumtafuta kwa udi na uvumba hatimaye alipata kipenzi chake akiwa amepoteza fahamu kutufuatia kiasi kikubwa cha chang'aa ambacho alikuwa amebwagia mdomoni.

Hapo ndipo kizaazaa kikubwa kilianza na kwa hasira Onyango akampiga mkewe vibaya kisha akambeba kwa toroli hadi nyumbani kwao.

Inaripotiwa kuwa baadae usiku wa Jumamosi Bi.Mayavi aliaga dunia kufuatia matatizo ya mwili ambayo alipata kutokana na kichapo kikubwa  alichopokea.

Polisi kutoka kituo cha Sihay walimkamata mshukiwa na anatarajiwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.