Kanisa la Katoliki lapiga marufuku hotuba za wanasiasa kanisani

Muhtasari

•Mwenyekiti wa baraza la waumini, Askofu Mkuu Antony Muheria amewaagiza wanasiasa kuenda kanisani kuhudhuria ibada tu kisha kuondoka kama waumini wengine.

•Muheria amewaomba  wanasiasa hao kuzungumza na Mungu wala sio waumini kila wanapoenda kuabudu kanisani.

Archbishop Antony Muheria
Archbishop Antony Muheria
Image: EUTYCAS MUCHIR

Kanisa la Katoliki limepiga marufuku wanasiasa wote nchini kuhutubia watu kanisani wakati wa ibada.

Mwenyekiti wa baraza la waumini, Askofu Mkuu Antony Muheria amewaagiza wanasiasa kuenda kanisani kuhudhuria ibada tu kisha kuondoka kama waumini wengine.

Muheria amewaomba wanasiasa kupatia kanisa heshima na kuwaeleza  kwamba watachukuliwa tu kama waumini wengine pale kanisani.

"Kanisa la Katoliki limesema kuwa halitaruhusu wanasiasa kuzungumza katika kanisa zetu. Wanasiasa ikiwa mnakuja kuabudu katika kanisa zetu mko karibu. Kaeni kama waumini wengine na tafadhali msitarajie kuhutubia watu. Tafadhali njooni muabudu kisha muende" Muheria amesema.

Askofu huyo amesema kwamba inasikitisha  kuona kuwa kuna baadhi ya wanasiasa ambao wanalazimisha kupewa nafasi ya kuhutubia waumini kila wanapoenda kanisani.

Muheria amewaomba  wanasiasa hao kuzungumza na Mungu wala sio waumini kila wanapoenda kuabudu kanisani.

"Mungu na wewe, anajua unachohitaji. Nenda kwake, usije kwetu. Usitake tukusifu, tafuta baraka za Mungu kivyako kama mtu mwingine yeyote. Acha tupatie nyumba ya Mungu na mahali takatifu heshima. Patwa na aibu wakati unaposimama pale kuzungumza siasa na matusi kwani unaalika laana maishani mwako. Huu ni ujumbe kwa wanasiasa wote" Askofu mkuu Muheria amesema.

Askofu huyo amewaomba maaskofu wengine haswa katika eneo la Nyeri anakohudumu kuwa imara katika utekelezaji wa agizo la kutowaruhusu wanasiasa kuzungumza kanisani.