Mwanamke ashirikiana na kijana kutapeli mumewe akidai kwamba ametekwa nyara na watu waliotaka 200,000

Wairimu alidai kwamba alitekwa nyara alipokuwa anatembea katika mtaa wa Loita jijini Nairobi

Muhtasari

•Usiku wa Ijumaa Mutuku alipokea simu kutoka kwa mkewe ambaye alimuarifu kwamba alikuwa ametekwa nyara na watu ambao walikuwa wanataka kulipwa shilingi laki mbili ili awachiliwe.

•Mutuku pamoja na familia ya Wairimu waliweza kuchanga shilingi 17,000 na kutumia 'watekaji nyara' wale ili kujaribu kuwashawishi wamuachilie.

•Kwa wakati huo Wairimu pamoja na Mogire walikuwa na Mogire kwa chumba chake katika mtaa wa Malaa ambako walikuwa wakijiburudisha.

crime scene
crime scene

Mwanamke anayedaiwa kushirikiana na kijana  kutapeli mumewe kwa kujifanya kwamba ametekwa nyara anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Embakasi.

Jane Wairimu anazuiliwa pamoja na Richard Mogire (21) ambaye walishirikiana naye kupanga njama ya kutapeli Bw Brian Mutuku. Mpenzi wa Mogire pia alikamatwa kwani alipatikana pamoja na wawili hao.

Kulingana na DCI, Wairimu alitoweka siku ya Ijumaa  wiki iliyopita  na kuacha mumewe akiwa amejawa na wasiwasi tele.

Usiku huo wa Ijumaa Mutuku alipokea simu kutoka kwa mkewe ambaye alimuarifu kwamba alikuwa ametekwa nyara na watu ambao walikuwa wanataka kulipwa shilingi laki mbili ili awachiliwe.

Wairimu alidai kwamba alitekwa nyara alipokuwa anatembea katika mtaa wa Loita jijini Nairobi.

Kufuatia hayo mume wa mshukiwa alipiga ripoti katika kituo cha DCI cha Embakasi kwamba mkewe alikuwa ametoweka.

Mutuku pamoja na familia ya Wairimu waliweza kuchanga shilingi 17,000 na kutumia 'watekaji nyara' wale ili kujaribu kuwashawishi wamuachilie.

Kwa wakati huo Wairimu pamoja na Mogire walikuwa na Mogire kwa chumba chake katika mtaa wa Malaa ambako walikuwa wakijiburudisha.

Kuona kwamba Wairimu hakuwa anarejea nyumbani, familia yake iliunda kikundi cha WhatsApp na wakachanga shilingi 40,000 zaidi ambazo walitumia 'watekaji nyara' wale siku ya Jumatatu.

Baada ya kupokea pesa zile kupitia Mpesa, Wairimu pamoja na Mogire walisafiri kutoka Malaa hadi Mtito-a-Ndei ambako walizitolea.

Mpenzi wa Mogire ambaye ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha JKUAT aliungana na wawili hao baada ya kusisitiza kuwa alikuwa anataka kumuona mpenzi wake. Haieleweki jinsi Mogire aliweza kushawishi mwanadada yule kukaa nao chumbani walikokuwa wamejificha.

Watatu hao wamekuwa wakikaa pamoja tangu siku ya Jumatatu hadi Jumatano ambapo walikamatwa katika maeneo ya Sagana.

Walipokamatwa, Wairimu alijitetea kwa kusema kuwa alikuwa ameamua kufanya vile ili kutorokea watu ambao alikuwa na madeni yao tangu apoteze kazi yake.