Hofu Kitale baada ya jamaa aliyekuwa ameenda kujisaidia kichakani kupata AK-47 iliyojaa risasi ikiwa imefichwa

Muhtasari

•Alipokuwa anathibisha tukio hilo, kamanda wa polisi katika kaunti ya Trans Nzoia Jacinta Wesonga alisema kwamba bunduki hiyo ilipatwa na jamaa aliyekuwa ameenda kujisaidia kichakani.

•Polisi waliofika kwenye eneo la tukio walithibitisha kwamba bunduki hiyo ilikuwa  na uwezo wa kufanya kazi na ilikuwa imejaa risasi.

AK-47
AK-47
Image: WIKIPEDIA

Hali ya hofu ilitanda  katika mji wa Kitale  baada ya bunduki aina ya AK-47 kupatikana ikiwa imeachwa kwenye kichaka kilicho karibu na klabu ya gofu ya Kitale siku ya Alhamisi.

Alipokuwa anathibisha tukio hilo, kamanda wa polisi katika kaunti ya Trans Nzoia Jacinta Wesonga alisema kwamba bunduki hiyo ilipatwa na jamaa aliyekuwa ameenda kujisaidia kichakani.

Inaripotiwa kwamba jamaa huyo aliona kitu kilichofanana na mtutu wa bunduki kikiwa kimetokelezea kutoka kwa karatasi ya plastiki iliyokuwa imefichwa na matawi ya mti.

"Jamaa huyo aliamua kuvuta kifaa hicho na kushtuka kuona ilikuwa bunduki aina ya AK 47" Bi Wesonga alisema.

Jamaa huyo alifahamisha meneja wa klabu ya Kitale ambaye alipiga ripoti kwa polisi.

Polisi waliofika kwenye eneo la tukio walithibitisha kwamba bunduki hiyo ilikuwa  na uwezo wa kufanya kazi na ilikuwa imejaa risasi.

Wesonga alimsifia jamaa aliyepiga ripoti baada ya kuona bunduki hiyo na kushauri umma kufahamisha maafisa wa usalama wanaposhuhudia tukio kama zile.