{Picha} Daktari Gakara pamoja na watoto wake wawili ambao anatuhumiwa kuua wazikwa

Muhtasari

•Bado haijabainiwa wazi kilichosababisha kifo cha watoto hao wawili huku mwanapatholojia Titus Ngulungu akisema kwamba matokeo ya upasiaji wa mwili ni yenye shaka.

•Alipokuwa anazungumza katika hafla ya mazishi, mjane wa marehemu Winnie Adhiambo alimsherehekea Gakara kama mwanaume shujaa mwenye "roho nzuri zaidi"

Mazishi ya Dkt Gakara na wanawe wawili katika kaunti ndogo ya Gilgil
Mazishi ya Dkt Gakara na wanawe wawili katika kaunti ndogo ya Gilgil
Image: BEN NDONGA

Daktari James Gakara anayetuhumiwa kuua watoto wake wawili kwa kuwadunga sindano yenye sumu kabla ya kujaribu kujitoa uhai, kisha kufariki akiwa hospitalini alizikwa siku ya Jumanne.

Gakara alizikwa kwenye kaburi moja ilhali watoto wake wawili Dylan (5) na Karuana (3) walizikwa pamoja kwenye kaburi moja nyumbani kwao katika eneo la Muririchwa kaunti ndogo ya Gilgil.

Rafiki mmoja wa familia alisema kwamba kulikuwa na mipango ya kuzika miili yote tatu kwenye kaburi moja ila wakabadilisha mawazo ili kupunguza saizi ya jiwe.(slab)

Hakuna mchanga ambao ulitupwa ndani ya kaburi baada ya majeneza kuwekwa ndani.

Familia na marafiki walijumuika uwanjani kufanya hafla ya mazishi kabla ya kuelekea kwa hafla ya kibinafsi nyumbani.

Alipokuwa anazungumza katika hafla ya mazishi, mjane wa marehemu Winnie Adhiambo alimsherehekea Gakara kama mwanaume shujaa mwenye "roho nzuri zaidi"

Alisimulia hadithi mbili azipendazo zaidi 'Punda kwenye kisima' na 'mbwa mwitu mbaya na nguruwe watatu wadogo' ambazo marehemu mumewe alipenda kusomea watoto wake.

Binti ya marehemu kutoka ndoa ya hapo awali, Agnes Njeri alisema kwamba Gakara alikuwa baba, mshauri na rafiki yake.

"Baba yangu alihakikisha nimepata masomo bora, nilifurahia kuwepo kwake na bila kujali kitakachofanyika, atabaki kuwa rafiki yangu" Njeri alisema.

Njeri alisema kwamba alifurahia wakati ambao walikuwa pamoja na ndgu zake marehemu Dylan na Karuana.

Gakara anatuhumiwa kudunga watoto wake sindano yenye sumu mnamo Septemba 18 nyumbani kwake mjini Nakuru kisha kujaribu kujitoa uhai kabla ya polisi kumpata akiwa amepoteza fahamu.

Hata hivyo alifariki mnamo Septemba 22 alipokuwa anahudumiwa hospitalini.

Mshauri wa Gakara, daktari Norman Njogu alimkumbuka kwani ndiye aliyempatia muongozo wa kazi yake.

Njogu alissema kwamba licha ya Gakara kuwa miongoni wa daktari wa uzazi bora zaidi alimchagua mwenyewe (Njogu) kusaidia mama yao kujifungua wanawe wawili.

"Nilijua Dylan na Hailey walipokuwa kwenye tumbo ya mama yao" Alisema.

Bado haijabainiwa wazi kilichosababisha kifo cha watoto hao wawili huku mwanapatholojia Titus Ngulungu akisema kwamba matokeo ya upasiaji wa mwili ni yenye shaka.

Sampuli zilipelekwa kwenye maabara ya serikali kwa uchunguzi zaidi.

Gakara alimiliki kliniki ya Optimum Current mjini Nakuru.

(Utafsiri: Samuel Maina)