Uhuru ampongeza Rais Mason, PM Motley kwa kuibadilisha Barbados kuwa jamhuri

Muhtasari
  • Katika taarifa, Uhuru pia amewapongeza Wananchi wa Jamhuri mpya ya Barbados
  • Alibainisha kuwa mpito huo ulikuwa ushuhuda wa azimio kubwa la watu wa Barbadia kupanga hatima yao wenyewe
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta Jumanne aliwapongeza Rais Dame Sandra Mason na Waziri Mkuu Mia Amor Motley kwa kugeuza nchi kuwa jamhuri.

Katika taarifa, Uhuru pia amewapongeza Wananchi wa Jamhuri mpya ya Barbados.

Alibainisha kuwa mpito huo ulikuwa ushuhuda wa azimio kubwa la watu wa Barbadia kupanga hatima yao wenyewe.

Mkuu wa Nchi, katika ujumbe wake alithibitisha utayarifu wa Kenya kuendelea kushirikiana na Jamhuri mpya ya Barbados katika kuendeleza Pan-Africanism.

"Wakati huohuo, Rais Kenyatta alimpongeza Mheshimiwa Dame Sandra Mason kwa kutwaa wadhifa wa juu wa Rais wa Jamhuri ya Barbados na kumtakia mafanikio anapoongoza Jamhuri mpya katika mustakabali wa ustawi," taarifa kutoka Ikulu ilisema.

Mwanamfalme wa Uingereza Charles na mwanamuziki Rihana walihudhuria warsha hiyo.

Kwenye hotuba Prince Charles alisema anaelewa dhuluma za utumwa zilizokumba kisiwa hicho cha Caribbean.

Kama ishara ya kubadilika kwa mamlaka, saluti ya mwisho ilipigwa kwa ufalme wa Uingereza na bendera ya kifalme kushushwa na nyingine kupandishwa.

Akiongea kama mgeni mkuu wa heshima , Prince Charles alisema uhusiano kati ya mataifa hayo mawili utaendelea licha ya kuwepo katiba tofauti.

Aliuelezea wakati huo kama mwanzo mpya kabla ya kupewa tuzo la juu la Barbados na rais mpya.

Malkia aliitakia nchi hiyo heri na fanaka, amani na maendeleo siku zinazokuja na kusema kuwa taifa hilo lina nafasi kubwa kwenye moyo wake.

Dame Sandra Mason, 72, Gavana mkuu wa kisiwa hicho tangu mwaka 2018 alitajwa kuwa rais.

Barbados ilitangaza mipango yake ya kuwa Jamhuri mwaka uliopita lakini bado itasalia katika kundi la nchi za jumuiya ya madola

Viongozi wakiwemo waziri mkuu walikula kiapo mbele ya rais mpya kwenye sherehe iliyodumu saa kadhaa.