Kinoti:Kuwa mwangalifu unaponunua bidhaa mitandaoni

Muhtasari
  • Katika taarifa, Kinoti alisema afisi yake imepokea malalamishi kutoka kwa watu walioagiza bidhaa mtandaoni lakini hazikuwasilishwa
Mkuu wa idara ya DCI George Kinoti
Mkuu wa idara ya DCI George Kinoti

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai George Kinoti amewataka Wakenya kuwa waangalifu wanaponunua bidhaa mitandaoni katika msimu huu wa sikukuu

Katika taarifa, Kinoti alisema afisi yake imepokea malalamishi kutoka kwa watu walioagiza bidhaa mtandaoni lakini hazikuwasilishwa.

Aliongeza kuwa wengine pia wamelalamikia ubora duni ikilinganishwa na ile inayotangazwa kwenye mitandao ya kijamii.

"Tumepokea ripoti nyingi kutoka kwa wateja ambao waliagiza bidhaa zinazotangazwa kwenye mitandao ya kijamii haswa kwenye Instagram, lakini bidhaa hizo hazikuwasilishwa au ubora haufanani na ule uliotangazwa," Kinoti alisema Jumatatu.

Kinoti alitoa wito kwa Wakenya kupinga vishawishi vya kutuma pesa kwa wanaodhaniwa kuwa wafanyabiashara wa kweli, ambao baadaye walibainika kuwa wabaya.

Pia alibainisha kuwa wahasiriwa wengi wa ulaghai huo wa mtandaoni ni wanawake ambao wako tayari kununua mavazi ya kisasa.

"Unashauriwa kuwa mwangalifu unapofanya ununuzi mtandaoni, kwa kufahamu kwanza utambulisho wa muuzaji na anwani ya biashara zao," Kinoti alisema.