Polisi kuchunguza tuhuma za kutekwa nyara kwa Dennis Itumbi

Muhtasari
  • Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu madai ya kutekwa nyara kwa mwanablogu na mtaalamu wa mikakati Dennis Itumbi
Image: EZEKIEL AMINGA

Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu madai ya kutekwa nyara kwa mwanablogu na mtaalamu wa mikakati Dennis Itumbi.

Itumbi, mshirika wa karibu wa Naibu Rais William Ruto, alidaiwa kutekwa nyara na watu wanaosemekana kuwa maafisa wa polisi mnamo Alhamisi huko Thindigua, kaunti ya Kiambu.

Katika taarifa siku ya Ijumaa, msemaji wa Polisi wa Kitaifa Bruno Shioso alisema kwamba suala hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Thindigua kupitia OB Nambari 10/23/12/2021 karibu saa 3.40 usiku.

Shioso aliwataka wananchi kuwa na subira wakati mamlaka inachunguza suala hilo.

Aliwataka waache kubahatisha.

Msemaji huyo pia aliwataka wale ambao wanaweza kuwa na taarifa za suala hilo kuripoti katika kituo chochote cha polisi au kupitia nambari za simu za 999, 112 na 080 722 203.

Mwanablogu wakati huo alikuwa uchi kabisa na alikuwa amevunjika miguu, mkono wa kushoto na alikuwa amechubuka jicho lake la kushoto.

Kulingana na kakake, David Itumbi, mwanablogu huyo ambaye hakwepeki kukosoa watendaji wa serikali alitekwa nyara na maafisa wa polisi ambao walimfanya aamini kwamba alikuwa Eldoret.

“Ndugu yangu amepigwa vibaya sana. Tunamshukuru Mungu kwamba yuko hai. Kwa akaunti yake mwenyewe alikamatwa na polisi na kupigwa na kuteswa. Hii ndiyo hali tuliyomkuta nayo,” alisema David.