Mfanyibiashara Mary Wambui ameachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 baada ya shtaka la kumiliki bunduki kinyume cha sheria

Muhtasari
  • Mfanyibiashara Mary Wambui ameachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 baada ya shtaka la kumiliki bunduki kinyume cha sheria
  • Upande wa mashtaka haukupinga kuachiliwa kwake kwa dhamana
Mfanyabiashara Mary Wambui. Picha: KWA HISANI
Mfanyabiashara Mary Wambui. Picha: KWA HISANI

Mfanyibiashara Mary Wambui alishtakiwa Alhamisi kwa kumiliki bunduki kinyume cha sheria kufuatia kukamatwa kwake Jumatano.

Wambui ambaye alifikishwa mbele ya hakimu mkuu wa Milimani Wendy Kagendo pia alikabiliwa na shtaka la pili la kumiliki bunduki bila leseni.

Alikanusha mashtaka yote mawili na kuachiliwa kwa bondi ya Sh100,000 kwa dhamana mbadala ya Sh50,000.

Upande wa mashtaka haukupinga kuachiliwa kwake kwa dhamana.

Mawakili wa Wambui, Nelson Havi na Kipchumba Murkomen awali walikuwa wameomba mahakama imwachilie mteja wao kwa dhamana ya Sh5, 000.

"Kosa ambalo mteja wangu amefikishwa mahakamani ni utovu wa nidhamu na ni upuuzi kwamba alilazimika kulala seli usiku kucha," Havi alisema.

Kesi hiyo itatajwa Januari 25.

Wambui alikamatwa Jumatano kwa madai ya kumiliki bunduki ambayo haijasajiliwa.

Wambui alichukuliwa kutoka nyumbani kwake Runda na kuhojiwa na maafisa wa upelelezi kabla ya kufikishwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga alikolala.

Mfanyibiashara huyo tayari anakabiliwa na shtaka la kukwepa kulipa ushuru wa Sh2.2 bilioni.

Uamuzi wa kukamatwa ulitolewa aliposalimisha bastola yake Desemba 15 mwaka jana, siku moja baada ya Bodi ya Leseni ya Silaha kusema alishikilia bastola hiyo kinyume cha sheria.

Leseni ilikuwa imeisha muda wake Aprili 17, 2020.