Lazima Raila Odinga akomeshe vurugu-DP Ruto awambia kinara wa ODM

Muhtasari
  • Ruto alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani hawezi kuendelea kutoa visingizio kuhusu ghasia
Naibu Rais William Ruto akihitubia wakazi wa Kangundo kaunti ya Machakos Alhamisi Januari 20/2022
Image: Geroge Owiti

Kiongozi wa ODM Raila Odinga lazima akomeshe vurugu, Naibu Rais William Ruto amesema.

Ruto alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani hawezi kuendelea kutoa visingizio kuhusu ghasia.

"Ninataka kuwaambia wale ambao tunashindana nao, tunataka kuhakikisha kuwa katika mlingano wetu wa uchaguzi hakuna vurugu," Ruto alisema.

Ruto alizungumza wakati wa mkutano wa hadhara wa UDA katika Mji wa Kangundo katika Kaunti ya Machakos Alhamisi.

"Na ninataka kuuliza ODM kumaliza ghasia. Na kiongozi wa ODM lazima akomeshe vurugu. Hawezi kuendelea kutoa visingizio kuhusu ghasia," Ruto alisema.

Alisema ghasia haziwezi kuongeza kura zozote nchini Kenya tena.

Ruto aliongeza, "Na wale ambao wana rekodi ya ghasia lazima watupe ahadi na kuwapa watu wa Kenya ahadi kwamba hawatatumia vurugu katika kampeni hizi na watakaposhindwa katika uchaguzi wa Agosti 9."

"Lazima wajitolee kwamba watakubali uamuzi wa watu wa Kenya, na hawatajiapisha wenyewe na hawataandaa maandamano," alisema.

"Wataegesha mabegi yao madogo na kwenda nyumbani."

Alisema lazima wamwambie Raila na kikosi chake cha ODM waache vurugu.

"Lazima tumwambie bwana kitendawili aache fujo. Amepanga fujo Kondele tukapigwa mawe. Amepanga fujo Embakasi tumepigwa mawe," Ruto alisema.

Aliendelea, "Mimi nataka nimwambie bwana Kitendawili mawe ni ya kujenga nyumba. Wacha kubebesha vijana mawe wapigane, tafuta sera."

Ruto alisema Raila anafaa kutafuta manifesto nyingine.

"Na nikiweza kukushauri, tafuta ilani nyingine. Acha mikono, mikono na mawe haviwezi kukupa kura."

Ruto alisema Wakenya wanataka uchaguzi wa amani.

Alisema Wakenya hawapaswi kupigwa mawe ili wapige kura, wana akili na hakuna mtu atakayewalazimisha kufanya maamuzi ya kupiga kura.

"Sio lazima uwalazimishe," aliongeza.

DP alitangaza chama chake cha UDA katika ziara yake katika miji ya Oldonyo Sabuk, Tala, Kangundo, Kivaani, Kakuyuni, Kathiani, Mitaboni na Joska katika Kaunti ya Machakos.

Alisema chama hicho kimeunganishwa na wabunge 160 walioamua kuunganisha nchi.

"Tunataka kuunganisha Kenya na Johnson Muthama ndiye mwenyekiti wa chama ambacho tayari kimevutia wabunge 160," Ruto alisema.

Aliwataka Wakenya kutokubali kugawanyika kwa sababu ya tofauti za kisiasa zinazosema kuwa umoja ni nguvu.

"Tunataka kuunda Kenya ambayo haina ubaguzi. Unganeni, fanyeni kazi pamoja na kuunda serikali ambayo itahudumia kila mtu. Tengeneza ajira kwa vijana na kukuza biashara," alisema.