Kawangware:Mwanabodaboda afariki baada ya kudungwa kisu na wezi

Muhtasari
  •  Mwendesha boda boda mmoja eneo la Kawangware jijini Nairobi alipoteza Maisha yake Jumatano alasiri baada ya kudungwa kisu na wanaume wawili katika kile kinatajwa kuwa ni tukio la kujaribu kuiba pikipiki yake.
  • •Katika mazingira ya kuvutana baina yao, mwizi mmoja alichechemea kutoka kwa pikipiki hiyo na kuchana mbuga baada ya wanabodaboda wengine waliojawa na ghadhabu kufika katika eneo la tukio na kumkamata mmoja ambaye alikiona cha mtema kuni.
Crime scene
Crime scene
Image: HISANI

Mwendesha boda boda mmoja eneo la Kawangware jijini Nairobi alipoteza Maisha yake Jumatano alasiri baada ya kudungwa kisu na wanaume wawili katika kile kinatajwa kuwa ni tukio la kujaribu kuiba pikipiki yake.

Mwanaume huyo, 31, ambaye wenyeji wa mtaa huo walimtambua kwa jina Mogaka Chacha ni mfanyibiashara wa bodaboda katika maeneo ya Kawangware na Kangemi na alikutana na mauti baada ya wezi hao wawili kujifanya wateja waliotaka kupewa huduma za usafiri kuelekea Kawangware 56.

Baada ya kufikia maeneo ya muslim wateja hao walimgeukia Mogaka na kumdunga visu mara kadhaa huku wakijaribu kuchukua udhibiti wa pikipiki yake.

Kulingana na ripoti ya maafisa wa upelelezi DCI, marehemu hakuwa tayari kuachia pikipiki yake, jambo ambalo lilisababisha mvutano kwa muda baina yake na wezi hao huku akipiga kamsa, jambo lililopelekea bodaboda wenzake kufika kumpa msaada.

“Katika mazingira ya kuvutana baina yao, mwizi mmoja alichechemea kutoka kwa pikipiki hiyo na kuchana mbuga baada ya wanabodaboda wengine waliojawa na ghadhabu kufika katika eneo la tukio na kumkamata mmoja ambaye alikiona cha mtema kuni.

Maafisa wa polisi kutoka kituo cha Muthangari walifika na kumuokoa mwizi huyo kutoka mikononi mwa wanabodaboda hao wenye hasira na hamaki,” DCI ilisema.

Mwizi huyo aliyenusurika kifo kwa sasa anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta huku maafisa wa upelelezi katika eneo bunge la Dagoretti wakiendeleza msako wa kumpata mwizi wa pili aliyetoroka kwa kuchechemea.