UDA haina makubaliano ya muungano na ANC, Ford-K - Muthama asema

Muhtasari
  • seneta huyo wa zamani wa Machakos aliwaambia wafuasi wake kupuuza ripoti za vyombo vya habari kuhusu makubaliano
Johnson Muthama
Image: Mercy Mumo

Chama cha UDA kimefafanua  kuwa hakina makubaliano ya muungano na ANC ya Musalia Mudavadi na Ford Kenya ya Moses Wetangula ikitupilia mbali ripoti za mpango wa kugawana mamlaka.

Mwenyekiti  wa UDA Johnson Muthama Jumatatu alisema hakuna makubaliano yaliyotiwa saini kati ya vyama vya siasa na kwamba kwa sasa vinaendesha shughuli zao kwa misingi ya urafiki.

Akihutubia kikao na wanahabari katika Ofisi yake  huko Gigiri siku ya Jumatatu, seneta huyo wa zamani wa Machakos aliwaambia wafuasi wake kupuuza ripoti za vyombo vya habari kuhusu makubaliano katika muungano changa wa Kenya Kwanza.

"Tunavyozungumza sasa, unahakikishiwa na si mwingine ila mwenyekiti wa UDA, hakuna makubaliano ya muungano ambayo yamefikiwa kati ya vyama vitatu vya muungano," Muthama alisema.

"Sisi ni marafiki ambao tunaendelea kuzungumza na kushirikisha lakini wakati ukifika basi suala hilo litashughulikiwa wakati huo." Muthama alikuwa akijibu ripoti kwamba makubaliano yametiwa wino kugawa baadhi ya kaunti na kuruhusu ANC na Ford Kenya pekee kusimamisha wagombea katika maeneo hayo.

UDA Jumapili ilitoa wito kwa umma kupuuza ripoti zinazoeleza jinsi chama hicho kinavyopanga kugawana nyadhifa za madaraka iwapo kitaunda serikali ijayo mwezi Agosti.