RIP: Ruben Kigame amuomboleza babake

Muhtasari

• Muimbaji mkongwe na injili na mwanasiasa Ruben Kigame anaomboleza kifo cha babake mzazi kilichotokea Februari 13. 

• “Nenda salama baba. Nitafanya kila niwezalo ili kukufanya ujivunie," ameandika Kigame

Image: REUBEN KIGAME

Muimbaji mkongwe na injili na mwanasiasa Ruben Kigame anaomboleza kifo cha babake mzazi kilichotokea Februari 13. 

Kigame ambaye pia alitangaza kujitosa katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2022 ameandika kwenye mitandao yake ya kijamii kwamba babake mzazi Richard amefariki dunia katika umri wake wa uzeeni kabisa. 

Amemuomboleza kuwa baba mwema maishani mwake ambaye alimpa maisha ya kimwili na amesema kwamba hata kama alikuwa mzee sana lakini bado hawakuwa tayari kutenganishwa naye kwa umauti. 

“Ayubu 1:21, Mungu ndiye mpaji na Mungu amechukua...Lihimidiwe jina lake. Ni kwa uchungu na huzuni mwingi kwamba ninamuaga mtu aliyenipa uhai wa kimwili. Kwaheri baba. Hata katika umri wa uzeeni, bado ni vigumu kukuachia uende,” ameomboleza Kigame 

Amesema kwamba babake alikuwa katika uchungu mwingi kabla ya kifo chake na familia ilijaribu kila namna kuokoa maisha yake lakini ikashindikana. 

“Nenda salama baba. Nitafanya kila niwezalo ili kukufanya ujivunie. Unajua vizuri nitamtunza mama pamoja na familia yote kwa ujasiri ulionifunza siku zote kuwa nao. Chenda bulahi papa!”