"Mbona Sonko? Mbona sasa?" Mike Sonko avunja kimya baada ya kupigwa marufuku kuingia Marekani

Muhtasari

•Katika taarifa iliyotolewa Jumanne jioni, Sonko alisema alishangazwa na hatua hiyo na kuihusisha na siasa.

•Ametoa ombi kwa Marekani kumchunguza balozi wake nchini Kenya na kuangazia katika kupambana na rai wa Russia Vladmir Putin badala ya kutumiwa kuhujumu azma yake ya kisiasa

Gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko
Gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko
Image: MAKTABA

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Gideon Mbuvi Kioko almaarufu Mike Sonko amesema hatua ya kupigwa marufuku kuingia Marekani ni njama ya kumnyamazisha na kuhujumu azma yake ya siasa.

Sonko alitoa taarifa baada ya Marekani kusema yeye na familia yake hawaruhusiwi kukanyaga huko kwa madai ya ufisadi 'mkubwa' alipokuwa mamlakani.

"Kwa nini Sonko, kwa nini sasa, miezi michache tu kabla ya uchaguzi mkuu? Nimepokea habari hizo  kwa mshtuko na kutoamini. Sitawahi kuogopa. Je, mimi ndiye mwanasiasa pekee anayekabiliwa na kesi ya ufisadi nchini Kenya?"  Sonko alisema.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne jioni, Sonko alisema alishangazwa na hatua hiyo na kuihusisha na siasa.

"Hatua hiyo bila shaka imechochewa kisiasa na wapinzani wangu wa kisiasaili  kuninyima haki yangu kama Raia wa Kenya kuthibitisha kwamba kwa kweli sina hatia," alisema.

Sonko alisema mahakama haijawahi kumpata na hatia yoyote katika kesi za ufisadi zinazomkabili.

Sijatiwa hatiani kwa mashtaka yoyote yanayohusiana na ufisadi kwa sababu kesi bado ziko mahakamani zikisubiri hukumu. Kuna magavana wawili pekee ambao wameshtakiwa katika mahakama ya sheria kwa kupatia wake zao na watoto zabuni lakini sio mimi. Hakuna hata mmoja wa wanafamilia wangu aliyewahi kupewa zabuni yoyote na kaunti nilipokuwa ofisini na iko hadharani, ubalozi unafaa kujitokeza hadharani na kuwaambia Wakenya ukweli. Mke wangu na watoto hawajawahi kuuzia City Hall hata kijiko au karatasi ya choo  moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja," Sonko alilalamika.

Sonko ametoa ombi kwa Marekani kumchunguza balozi wake nchini Kenya na kuangazia katika kupambana na rai wa Russia Vladmir Putin badala ya kutumiwa kuhujumu azma yake ya kisiasa