Wanawake wanyonyeshe watoto, marufuku kutumia chupa! - Serikali yaamuru

Muhtasari

• Chuchu anazolishwa mtoto hutengenezwa kwa silikoni ambayo haina mwonekano sawa na titi na hii huleta mkanganyiko na kusababisha mtoto kukataa kunyonya - Esther Mogusu, Afisa wa lishe wa NMS.

Image: THE STAR

Serikali ya Kenya Jumatano ilitangaza kupigwa marufuku kwa matumizi ya chupa za kunyonyesha watoto, kwanzia mwisho wa mwezi wa tano.

Afisa mkuu wa lishe katika bodi ya NMS Esther Mogusu akizungumza na wajumbe katika kongamano la kitaifa la lishe ya mama na watoto wachangaalifurahikia tangazo hilo la serikali kwa kile alisema kwamba chupa hizo mbadala kwa matiti ya kina mama zina mathara mengi kuliko mazuri.

“Sababu ya kudhibitiwa ni vitu vyovyote vinayolishwa kwa mtoto kwa kutumia chupa sio maziwa ya mama, lakini mara nyingi yatakuwa maji yasiyo ya lishe. Chuchu anazolishwa mtoto hutengenezwa kwa silikoni ambayo haina mwonekano sawa na titi na hii huleta mkanganyiko na kusababisha mtoto kukataa kunyonya,” alieleza kituo kimoja cha runinga nchini.

Akitoa tangazo la usitishwaji wa matumizi ya chupa hizo kwanzia Mei 28, mkurugenzi wa afya lishe bora katika wizara ya afya, Veronica Kirogo alisema kwamba marufuku hiyo haimaanishi kuathiri uzalishaji wa vyakula vya watoto ila tu ni kudhibiti uuzwaji wake.

“Nakubaliana kabisa na marufuku hiyo, lakini inapaswa kuja na miongozo kwa sababu bila mafunzo, habari na njia mbadala, hakutakuwa na uzingatiaji,” aliongeza Martha Nyagaya ambaye ni mkurugenzi katika Nutrition International.