(Video) KRA kubadilishwa jina hadi KRS, Waziri Yatani adokeza

Muhtasari

• "Ninapendekeza kufanyiwa marekebisho sheria ya mamlaka ya kutoza ushuru KRA ili kubadilishwa jina kwenda lile la huduma ya watoza ushuru KRS,” - Yatani

Waziri wa fedha Ukur Yatani amedokeza kwamba huenda mamlaka ya ukusanyaji kodi ya KRA ikabadilishwa jina na kuitwa mamlaka ya kutoa huduma kwa walipa kodi yaani Kenya Revenue Service, KRS.

Akizungumza Alhamis wakati wa kusoma bajeti ya mwaka 2022-2023, bajeti ambayo pia inaandikisha historia kuwa kubwa zaidi na ya mwisho kwa utawala wa serikali ya Jubilee, Yatani alisema kwamba hatua hiyo itakuwa ni mojawapo ya mageuzi yanayolenga kuboresha taasisi hiyo ya serikali ili kuwapa faida walipa ushuru, na pia kuwiana na mageuzi yanayoambatana na mambo mapya ya kidijitali.

“Ili kuiweka mamlaka hii ya ukusanyaji ushuru katika mkondo sawia na mambo mapya yanayochipukia kidijitali, ninapendekeza kufanyiwa marekebisho sheria ya mamlaka ya kutoza ushuru KRA ili kubadilishwa jina kwenda lile la huduma ya watoza ushuru KRS,” Waziri Yatani alidokeza.

Alielezea kwamba mamlaka hiyo tangu kukumbatia utoaji huduma za kidijitali, imekuwa ikijiandaa vizuri na hivyo ni vizuri iitwe ni mamlaka ya kutoa huduma.

“Mashirika ya serikali yanatarajiwa kuwa nyeti na kuitikia mahitaji ya wateja wanaojitokeza. Kuhusiana na hili, Mamlaka ya KRA imekuwa katika safari ya mageuzi ili kuimarisha utoaji wa huduma unaozingatia wateja,” alielezea waziri Yatani.