Mrengo wa Ruto waikosoa bajeti ya 2022-23, Mbunge Ndindi Nyoro asema takwimu ni za uongo

Muhtasari

• “Hii bajeti iko mbali sana na mwananchi wa kawaida nac kama nilivyoshikilia hapo awali, bajeti hii iko na mapungufu mengi sana" - Ndindi Nyoro

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro
Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro
Image: Facebook

Mrengo wa Kenya Kwanza kama ilivyotarajiwa tayari umeikosoa vikali bajeti ya mwaka 2022-23 iliyosomwa bungeni Alhamis na Waziri wa fedha Ukur Yatani.

Akizungumza nje ya bunge pindi baada ya bajeti hiyo kusomwa, mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro alisema bajeti hiyo iko mbali sana na maslahi ya mwananchi wa kawaida na kuzikosoa takwimu zote za Ukur Yatani kuwa mambo ya kufikirika tu wala hayana mashiko yoyote.

“Hii bajeti iko mbali sana na mwananchi wa kawaida nac kama nilivyoshikilia hapo awali, bajeti hii iko na mapungufu mengi sana. Takwimu ambazo alipatiana kulingana na ukuaji wa GDP wala haziendani kabisa. Mwaka wa 2013, GDP ya kenya ilikuwa takribani dola bilioni 55 (KSH 6.3T). Mwaka jana kama utairejelea hotuba yake, alidai kwamba GDP ya Kenya ilikuwa takribani dola bilioni 100 (KSH 11.5T), halafu leo anasema kwamba GDP ya Kenya iko dola bilioni 135 (KSH 15.4T), hiyo inamaanisha nini? Kwamba kama mwaka jana ilikuwa dola bilioni 100, na sasa hivi n idola bilioni 135, basi uchumi wa taifa umekuwa kwa kasi ya asilimia 35, kama si hivyo basi itakuwa kulikuwepo na mambo fulani ambayo tulifichwa,” alisema Nyoro.