Wacha Pasaka ituunganishe-Ujumbe wa Raila wa Pasaka kwa wakenya

Muhtasari
  • Alisema Pasaka ni kielelezo tosha kwamba wakati wa mwanadamu duniani ni mdogo
Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Mwanaiaji wa urais katika vuguvugu la Azimio Raila Odinga ametoa wito kwa Wakenya kuungana katika ari ya Pasaka kwa manufaa ya wote nchini.

Kupitia ujumbe wa video kwenye Twitter Jumamosi, Raila aliwataka Wakenya kuiga ushujaa ambao Yesu Kristo alikabili kifo nao na kusalia na umoja kati ya hali inayokabili nchi kwa sasa.

Alisema kwa vile Pasaka imekuja katika wakati mgumu, imetufundisha faida za ujasiri, uadilifu, upendo na huruma jinsi Yesu alivyodhihirisha hata alipokabiliwa na kifo kikubwa.

"Unaposoma Biblia, inakukumbusha jinsi Yesu alivyowasilishwa mbele ya Pilato, Warumi walikuwa wamemshtaki kwa kukufuru kwa kudai kuwa mwana wa Mungu. Yesu hakuwahi kujitetea...hakuogopa kifo,” Raila alisema.

Alisema ikiwa Wakenya wote wataiga ushujaa usio na kifani ulioonyeshwa na Yesu, hakuna changamoto ambayo nchi haiwezi kuikabili.

"Kama Wakenya, tukiungana pamoja, hakuna tunachoweza kushinda au kufanikisha. Tunasherehekea Pasaka katika wakati mgumu lakini haya yote yatapita," Raila alisema.

Kiongozi huyo wa ODM alisema ni lengo hili hasa la kuunganisha nchi katika hali ya dhiki lililofahamisha kubuniwa kwa vuguvugu la Azimio la Umoja.

"Tunataka mwanzo mpya...ili tuafiki ndoto za mababu zetu," Raila alisema.

Alisema Pasaka ni kielelezo tosha kwamba wakati wa mwanadamu duniani ni mdogo.

Pasaka, ambayo pia huitwa umapili ya Ufufuo, ni sikukuu ya Kikristo na sikukuu ya kitamaduni inayoadhimisha kufufuka kwa Yesu kutoka kwa wafu.

Inaelezwa katika Agano Jipya kama ilitokea siku ya tatu baada ya kuzikwa kwake kufuatia kusulubishwa kwake na Warumi pale Kalvari.

Kifo cha Yesu kinaadhimishwa na Wakristo siku ya Ijumaa Kuu.