Ruto sio 'hustler' wa ukweli-Jimi Wanjigi asema

Muhtasari
  • Mfanyibiashara huyo pia alimkashifu Uhuru akidai kuwa anakopa kila mwezi ili kukidhi nakisi ya bajeti
Jimi Wanjigi akizungumza baada ya kujiunga na chama cha Safina 9/Machi/2022
Image: Ezekiel Aming'a

Mwaniaji urais Jimmy Wanjigi amemdharau Naibu Rais William Ruto kuhusu manifesto yake akisema anawahadaa Wakenya.

Akiwa katika kampeni zake, Wanjigi alisema ajenda ya DP kwa Kenya si ya kweli.

"Ruto si 'hustler'wa kweli kwa sababu mtu wake (aliyekuwa Waziri wa Hazina Henry Rotich) ndiye aliyesimamia makosa ya kiuchumi ambayo yanawalemea Wakenya kwa sasa," Wanjigi alisema.

Wanjigi alizungumza Jumapili katika Kaunti ya Kwale baada ya kukutana na jamii ya Wamakonde huko Guasi.

Mwaniaji huyo wa urais wa Chama cha Safina alisema Wakenya wote wana haki ya kusikilizwa na kuwakilishwa licha ya wingi wa watu.

Mfanyibiashara huyo pia alimkashifu Uhuru akidai kuwa anakopa kila mwezi ili kukidhi nakisi ya bajeti.

“Rais Mstaafu Mwai Kibaki aliacha ulipaji wa deni letu kwa Sh10 kati ya kila Sh100 ya mapato yetu yaliyokusanywa. Lakini Rais Uhuru Kenyatta ametuhamisha hadi Sh75 kati ya Sh100 za mapato yaliyokusanywa.”

Hapo awali, mfanyabiashara huyo alimwomba rais kustaafu kwa amani baada ya kumaliza muhula wake wa pili na wa mwisho madarakani na akome kuingilia uchaguzi mkuu wa Agosti.

Wanjigi alisema mkataba wa muungano huo uliotiwa saini na muungano wa Azimio ni dhibitisho kuwa Uhuru bado anataka kushawishi maamuzi ya serikali baada ya kuondoka madarakani.

"Shukrani zako ni kama za punda anayerusha mateke, nenda nyumbani hatutaki kukuona tena, ondoka tu kwetu, nenda zako na uondoke kabisa," alisema.

Alisema kuwa safari yake hadi Ikulu chini ya chama cha Safina haikuwa na kikomo, akithibitisha kuwa muungano aliokuwa akiunda utakuwa wazi kwa Wakenya na sio wa kikabila au kwa msingi wa kuunda nyadhifa.