Washukiwa 4 wakamatwa kwa madai ya kuwapa abiria 'mchele' kwenye basi ili kuwaibia

Muhtasari
  • Baada ya kuona kuna kitu kibaya, Barasa alichukua mkondo hadi kituo cha polisi cha Kabete
Pingu
Image: Radio Jambo

Washukiwa wanne wamekamatwa kwa kuripotiwa kuwawekea abiria  dawa ya kulala ndani ya basi lililokuwa likielekea Nairobi  ili kuwaibia.

Stephen Odero, Benson Odero, Joshua Orengo, na Harrison Nyamu wanadaiwa kupanda basi hilo mjini Kisumu siku ya Jumapili kwa nia ya kutekeleza uhalifu huo.

Dereva wa basi hilo, Emmanuel Barasa, alishuhudia hali isiyo ya kawaida kwenye basi hilo ambapo kila mtu alikuwa amelala fofofo isipokuwa abiria wawili ambao walibadilishana nafasi.

Baada ya kuona kuna kitu kibaya, Barasa alichukua mkondo hadi kituo cha polisi cha Kabete ambapo mipango ya kutoroka ya washukiwa wawili ilitatizwa.

"Jaribio la majambazi hao wawili kuruka kutoka kwenye basi hilo lililokuwa likienda kwa kasi liliambulia patupu, baada ya dereva huyo kuvamia kituo cha polisi kwa mwendo wa kasi na kuwafanya maafisa wa polisi waliokuwa katika zamu ya ulinzi kukimbilia mahali pa kujificha na kuchukua nafasi, endapo kutatokea jambo lolote."

Kulingana na DCI, wakati wa ukaguzi, wapelelezi wa polisi walibaini kuwa idadi kubwa ya abiria walikuwa na vitu  kama vile kompyuta ndogo, kompyuta za mkononi, simu za rununu na pesa.

Wanne hao walikamatwa baada ya kupatikana wakiwa na vitu vilivyotoweka.

Hata hivyo, walikimbizwa hospitalini baada ya mamlaka kugundua kuwa walikuwa wamemeza dawa iliyosalia ili kuondoa ushahidi wowote.

"Ni hospitalini ambapo iligunduliwa kuwa washukiwa walikuwa wamekunywa dozi ya dawa zao wenyewe baada ya kumeza 'mchele'uliosalia, kwa nia ya kuharibu maonyesho," aliongeza Kinoti.

Basi hilo liliruhusiwa kuendelea na safari, lakini abiria walihimizwa kutafuta matibabu walipofika.

Wakati huo huo, washukiwa hao wanne bado wako rumande wakisubiri kufikishwa mahakamani leo.